Tuesday, 12 November 2013

“tuombe jina la Yesu kristo lisikike na kuwaokoa Wanakanisa na vitendo vya Kigaidi ambavyo vimekuwa vikiendana na mauaji yao, uchomaji moto wa makanisa pamoja uteketezaji wa mali za waumini wa kanisa”.



                                                                 FATHER CAMILUS

 Na Steven Augustino,Kitulila Njombe
 

“tuombe jina la Yesu kristo lisikike na kuwaokoa Wanakanisa na vitendo
vya Kigaidi ambavyo vimekuwa vikiendana na mauaji yao, uchomaji moto
wa makanisa pamoja uteketezaji wa mali za waumini wa kanisa”.
 

Wito huo ulitolewa na Asikofu wa jimbo la TUNDURU-Masasi mhashamu
Castory Msemwa wakati akiongea na  waumini wa kanisa katoliki wakati
akihubiri katika adhimisho la misa takatifu ya shukrani ya jubilei ya
kutimiza  miaka 25 ya upadre,miaka tisa ya uaskofu na miaka 58 ya
kuzaliwa kwake iliyofanyika katika kigango cha Mtulila parokia ya
Matola jimboni Njombe .
 

Akifafanua mahubiri hayo Askof Msemwa alisema kuwa hata kama Wakristo
ni wachache lakini aliwataka Wakristo kote nchini kushikamana na
kuombea kwa ajili ya miito mitakatifu ilikuongeza idadi ya watumishi
wa Kanisa kwamadai kwamba hivi sasa wanaojiunga katika utumishi wa
kanisa wanaendelea kupungua kwa kasi.
 

Alisema wakati yeye anatimiza miaka 25 ya upadre katika kigango chake
cha Mtulila na parokia nzima ya Matola  hakuna hata mseminari mmoja
ambaye yupo seminari kuu  hivyo  inahitajika kuendelea kuungana
kuomba kwa ajili ya miito.
 

“Siamini kama kweli hakuna vijana wanaoweza kujiunga na mito
mitakatifu katika ngazi ya kigango na parokia,tunahitaji sala katika
familia zetu,kama hatufanyi hivyo tuelewe wazi kuwa tunamkosea
mwenyezi Mungu,kila mmoja wetu amesalimiwa na Mungu lakini hatutaki
kuongea na Mungu,maana yake hatutaki kusali katika familia
zetu,hatutapata mapadre wala watawa’’,alisisitiza askof Msemwa.
 

Kufuatia hali hiyo akawatahadharisha waumini wa parokia ya Matola
yenye waumini zaidi ya 11,000  kutosahau alama zinazowafanya kuwa
wakristo zikiwemo kushindwa kutoa hadithi za Mungu na kutosali ndani
ya familia hali ambayo imesababisha watoto kutojua hata ishara ya
msalaba hadi wanapopata mafundisho katika shule za msingi hali
inayosababisha miito kuwa migumu.
 

Kwa mujibu wa Askofu Msemwa,wakati anapatiwa daraja takatifu mwaka
1987 katika kigango cha Kitulila pekee kulikuwa na watawa wa kike na
wa kiume 27 na kwamba watawa waliongezeka toka mwaka huo hadi sasa
hawazidi watawa 10 licha ya takwimu kuonyesha kuwa kuwa katika familia
kuna ongezeko kubwa la vijana.
 

Akizungumzia sababu za waumini wa kanisa katoliki kuhamia madhehebu
mengine yakiwemo ya kilokole,mhashamu Msemwa aliitaja sababu kubwa
inayochangia kuongezeka kwa tatizo hilo kuwa ni wazazi na walezi
katika familia wameanza kuzembea kusali kuacha kulea familia zao
katika misingi ya kanisa katoliki hivyo vijana kuamua kufuata yale
wanayoyaona yanapendeza katika masikio yao na kuamua kuokoka.
 

Aidha aliwashauri wazazi na walezi kuhakikisha kuwa mizizi ya imani ya
kanisa inaingia sawasawa kwa watoto wao ili waweze kuimarishwa zaidi
katika imani kwa kuwa ni vigumu kuingia mbinguni bila kuwa na imani
iliyokomaa ambayo inanzia katika ngazi ya familia na kwamba wazazi na
walezi waache kuwategemea makatekista kuimarisha imani.
 

 Naye Xavery Mlelwa paroko wa parokia ya Madunda ambaye amewahi pia
kuwa paroko katika kigango cha Kitulila alisema sehemu kubwa ya jimbo
la Njombe ikiwemo parokia ya Matola yenye waumini zaidi ya 11,000
asilimia kubwa ya watu ni wakristo hivyo akashauri kuwa ili lengo la
kufufua imani liweze kufanikiwa ni vema likaanzia ngazi ya familia.
 

“Ni kweli sisi tumelegea katika imani kwa kuwa hatuna changamoto
nyingine kama maeneo mengine ambayo yana waumini wa kiislamu,kumbe
ukiishi na mtu ambaye mmetofautiana kifikra au imani unaweza
kujiimarisha zaidi hivyo kwa kuwa tupo watu wa aina moja tumejisahau
na kushindwa kuilinda imani’’,alisema padre Mlelwa.
 

Wakiongea kwa nyakati tofauti Baadhi ya waumini na wanafamilia wa
mhashamu Askofu Msemwa walitoa maoni tofauti kuhusu jubilei ya miaka
25 ya upadre na miaka tisa ya uaskofu ambapo dada yake askofu Msemwa
ambaye ni mtawa wa shirika la Vinsent Sr.Lucia Msemwa alisema kaka
yake alionekana mapema kuwa anaweza kuwa mchungaji wa watu.
 

“Kaka yangu Askofu Msemwa ambaye ni mtoto wa nne kati ya watoto kumi
katika familia yetu,alikuwa anamsaidia baba kuchunga mifugo mbalimbali
 tangu akiwa shule ya msingi na aliendelea kuchunga hadi alipofikia
seminari kuu akirudi likizo alipenda kumsaidia baba kuchunga nadhani
alikuwa anaandaliwa kuwa mchungaji wa watu’’,alisema Sr.Lucia Msemwa
dada yake Askofu Msemwa.
 

Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa familia ya Askofu Msemwa tangu
awali ilijengwa katika imani iliyokomaa,kutokana na ukweli kuwa
kuanzia baba yake mzazi Askofu Msemwa  anayeitwa Paulonus Msemwa(93)
bado yupo hai alizaliwa mwaka 1920 katika maisha yake alikuwa mwalimu
wa dini (katekista) hivyo kuwalea watoto wake katika misingi ya imani.
Hali hiyo ndiyo ilimfanya mtoto wa kwanza wa mzee Msemwa aliyezaliwa
mwaka 1950 , Menas Msemwa  kufanyakazi ya ukatekista ,pia dada yake
 

Askofu Msemwa, Sr.Lucia Msemwa ni mtawa wa shirika la Vincent lakini
kubwa zaidi  familia hiyo kubahatika kutoa Askofu Desemba 7 mwaka 2004
baada ya Askofu Castory Msemwa kuteuliwa na Baba mtakatifu (Mstaafu
Paul wa XvI) kuwa Askofu wa jimbo la Tunduru-Msasi.
 

“Katika familia yetu tulipata malezi bora baba yetu mzazi alikuwa ni
mwalimu wa dini, mdogo wangu ni  Askofu  Msemwa,mimi mwenyewe nilikuwa
 katekista hadi nilipostaafu,dada yangu alikuwa kiongozi wa kanisa
katika parokia ya Matola,dada yangu mwingine ni sista katika shirika
la Vincent hadi sasa’’,alisema Menasi Msemwa kaka yake Askofu Castory
Msemwa.
 

Hata hivyo kaka huyo wa Askofu aliitaja siri kubwa iliyosababisha
Askofu Msemwa kupanda kwa haraka kutoka daraja takatifu la upadre hadi
kuteuliwa kuwa Askofu ni sala na maombi  na kwamba wazazi wao tangu
wakiwa wadogo waliwawekea msingi wa kusali sala mbalimbali ikiwemo
lozari kabla na baada ya kulala.
 

Baba mzazi wa Askofu Msemwa mzee Paulunus Msemwa alisema kuwa
amefurahia sana jubilei ya miaka 25 ya upadre wa mtoto wake, na kwamba
watoto wake aliwajenga katika misingi ya kiimani,hata hivyo alidai
kilichomfurahisha zaidi ni kuhojiwa,kupigwa picha na mwandishi wa
habari kwa kuwa katika maisha yake yote ya umri wa miaka 93 hajawahi
kuandikwa katika chombo chochote cha habari.
 

“Sijawahi mimi kuandikwa na chombo cha habari, kwa mara ya kwanza ni
leo tu,naona sasa wameona umuhimu wa familia hii kuandikwa na kuingia
kwenye historia ili wengine watakaosoma au kusikia kuhusu familia hii
waweze kujifunza hasa mambo ya  imani na kusali kuanzia ngazi ya
familia’’,alisisitiza mzee Msemwa.
 

Askofu Castory Msemwa alizaliwa Februari 13/1955 katika kigango cha
Kitulila parokia ya Matola jimbo la Njombe kwa wazazi Paulunus Msemwa
na Yulina Msemwa, alibatizwa katika Kijiji cha Uwemba mwaka 1955,
elimu ya msingi alisoma kuanzia mwaka 1968 hadi 1973 katika shule ya
msingi Matola,kidato cha nne sekondari ya Mafinga kati ya mwaka 1974
hadi 1977,alijiunga seminari ndogo ya Likonde kidato cha tano na sita
kati ya mwaka 1978 na 1980.
 

Mhashamu Msemwa mara baada ya kujiunga na mafunzo ya Jeshi la Kujenga
Taifa JKT ,alijiunga na seminari kuu Peramiho mwaka 1981,alipata
daraja takatifu la upadre mwaka 1987 na kuteuliwa na Baba mtakatifu
kuwa Askofu wa jimbo la Tunduru-Masasi mwaka 2004.
 

Mhashamu  Msemwa ambaye alifanya jubilei ya miaka 25 ya upadre mwaka
jana, amehitimisha adhimisho la misa ya shukrani ya Jubilei ya miaka
25 ya upadre wake mwaka huu katika kigango cha Kitulila parokia ya
Matola jimbo la Njombe ambako ni nyumbani kwake alikopatia daraja
takatifu la upadre.
 

Mhashamu Msemwa kuanzia Oktba 9 hadi 20 alifanya ziara katika parokia
saba kati ya 45 za jimbo la Njombe kwa lengo la kufanya misa za
shukrani kwa ajili ya Jubilei ya miaka 25 ya upadre wake .
Katika ziara hiyo ya misa ya shukrani ya jubilei ya miaka 25 ya upadre
mhashamu Msemwa ametoa sakramenti ya kipaimara kwa watoto 1258 kutoka
parokia saba za jimbo la Njombe.
 

Kati ya watoto hao parokia ya makete watoto 146,Ikonda watoto
115,Matola 275,Madunda 334,Kifanya 270,kigango cha Boimanda watoto 62
na kigango cha Kitulila ambacho amezaliwa askofu Msemwa ametoa
sakramenti ya kipaimara kwa watoto 56,amefungisha ndoa jozi tano na
kutoa ubatizo kwa watoto kadhaa.
Mwisho

No comments:

Post a Comment

TUPE MAONI YAKO