Maandishi yanampa msomaji picha ya halisi ya historia ya Makumbusho
ya maji maji yaliyopo katika mji wa Songea kusini mwa Tanzania.
Mkoa wa Ruvuma unapakana na nchi ya Msumbiji kwa upande wa
kusini,Kasikazini mkoa huu unapakana na mkoa wa Morogoro,Kaskazini-Magharibi
mkoa wa ruvuma unapakana na mkoa wa iringa.Magharibi mkoa huu unapakana na nchi
ya Malawi na kwa upande wa mashariki kuna mikoa ya Lindi na Mtwara.
Historia ya Makumbusho haya inahusu vita ya Maji Maji
vilivyo tokea kati ya mwenzi julai.1905 mpaka Agosti 1907.Vita hivi vilianza
katika vilima vya Umatumbi Kaskazini mwa mji wa Kilwa mnamo mwazi Julai mwaka
1905.
Waanzilishi wa awali wa vita hii walikuwa ni Wamatumbi chini
ya uhamasishaji wa Mganga wa jadi/Nabii aliye julikana kwa jina la Kinjeketile.Vita
hivi vilienea kama moto katika nyasi kavu na kusambaa katika makabila ya
Wamwera,Wangindo,Wapogoro,Wangoni,Wabena,Wasangu na wengineo. Watu hawa
walipigana kupinga kukandamizwa na kulazimishwa na wakoloni wa Kijerumani namna
ya kuishi,mazao ya kuzalisha na nani wa kumtumikia.
Picha ya Askari wa Kijerumani
Jina la vita hivi lilitokana na imani ya matumizi ya dawa
iliyochanganywa na Maji,punje za mahindi na mtama zilizosadikiwa kuwa zitampa
mpiganaji kinga ya kutodhurika kwa shambulio la risasi za majeshi ya Wajerumani.Inakadiriwa
watu 75,000 walipoteza maisha yao ukanda wa kusini mwa Tanzania baada ya vita.
Katika eneo la Ruvuma inakadiriwa kuwa zaidi ya watu 1,000 walipoteza maisha
yao.
Baada ya vita viongozi na askari walioshiriki katika vita
walikamatwa na kuhukumiwa kunyongwa mpaka kufa.Tarehe 27 February 1907 ilikuwa
siku ya masikitiko makubwa kwa watu wa Ruvuma
ambapo kadri ya watu 60 walinyongwa kwa sababu ya kushiriki katika vita.
Mashujaa hawa walinyongewa nyuma ya eneo ambalo leo hii linajulikana kama
“Songea Club”. Baada ya kunyongwa miili yao ilizikwa katika kaburi la
halaiki,lililoandaliwa na wafungwa kwa muda wa miezi miwili. Siku tatu baadaye
Chifu Songea alinyongwa na kuzikwa katika kaburi lililoandaliwa na kaburi la
halaiki.
Hili ndilo Kaburi la halaiki walipozikwa mashujaa wa vita vya Maji Maji , watu waliozikwa hapa ni 66
Eneo walilozikwa mashujaa hawa limekuwa eneo muhimu.
Tukio hili lilikuwa la huzuni sana kwa watu wetu hivyo watu
hawakulizungumza kwa kitambo kirefu. Baada ya uhuru (1961) Baadhi ya wazee
walianzisha harakati za kuwakumbuka mashujaa hawa. Walianza kufanya maombi yao na maadhimisho katika eneo
lililo karibu na eneo walilonyongewa wapiganaji hao.Shughuli hizi zilifanyika
katika nyumba ya Padre Chengula.
Wazo la kuwa na maadhimisho ya Kitaifa lilianzishwa na
kamati ya wazee wa kingoni.Walitoa taarifa kwa Mkuu wa mkoa Bw Martin Haule
aliyekuwa ameteuliwa wakati huo.Baadhi ya wazee waliokuwa katika kamati hii ni
pamoja na Xavery Zulu,Padrea
Chengula,Daudi Mbano,Ali Songea Mbano,Agatha Shawa,Alana Mbawa,Mwl Duwe,Shaibu
Mkeso na Daniel Gama.
Baada ya kuwasilishwa
wazo hili kwa Mheshimiwa Martin Haule,alichukua
hatua za dhati katika kulishughulikia jambo hili.Hatua ya kwanza ilikuwa
kutambuwa eneo ambalo mashujaa hawa walizikwa.
Eneo hili walipozikwa mashujaa lilitambuliwa na Bw Jumbe Darajani ambaye alishuhudia
tukio la kunyongwa kwa wahenga hawa(wakati wa utoto wake). Alama iliyotumika
kufahamu eneo hili ilikuwa ni mti mmoja uliojulikana kwa jina la CHIKUNGUTI.Baada ya kutambuwa eneo hili
mheshimiwa Haule alifanya uchimbuzi na kupata baadhi ya mifupa.
Kaburi la Songea Mbano ambaye alizikwa peke yake na jina la Mji wa Songea limetokana na jina lake
Kabla ya Bwana Haule kukamilisha kazi hii alihamishiwa mkoa
wa Ruvuma mwaka 1964.Wazo hili la kuwaenzi wahenga hawa liliibuka tena mwaka
1979 wakati Bw Laurence Gama
alipoteuliwa kuwa Mkuu wa mkoa wa Ruvuma.Aliendelea na jitihada za kutekeleza
wazo hili. Alianza kuhamasisha na
kutafuta Fedha kwa ajili ya ujenzi wa makumbusho kwa kushirikiana na wazee wa
Ruvuma na Wananchi wengine ujenzi wa jengo la makumbusho ulianza na kukamilika
mwaka 1980.
Pamoja na kukamilisha ujenzi wa jengo hili pia zilijengwa
sanamu katika eneo la mbele ya jengo.sanamu hizi zinajumuisha sanamu ya Askari
wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania,Mwl J.K Nyerere na sanamu 12 za machifu wa
kingoni.Lakini kwa sasa sanamu ya hayati Mwl J.K Nyerere imetolewa baada
yakuonekana haina kiwango cha juu hivyo inaandaliwa sana upya ili iweze kuwekwa
upya.Kazi ya kutengeneza sanamu hizi ilifanywa na msanii mmoja huko Arusha.
Vifaa vya awali katika Makumbusho haya vilikusanywa na
Mheshimiwa Laurence Gama, Padri Chengula na baadhi ya wazee. Vifaa vilivyokusanywa
vilijumuisha silaha zilizotumika wakati wa vita vya Maji Maji kama vile
Chikopa(Ngao), Chibonga(Rungu),Chinjenje(Kishoka), pia baadhi ya viti
vilivyotumiwa na Chifu Mputa, Vifaa vya ndani na nguo za magome ya Miti.
Kuanzia mwaka 1980 baraza la wazee lilianza kuadhimisha
maombolezo ya mashujaa walionyongwa kila ifikapo tarehe 27 Februari ya kila
Mwaka. Makumbusho haya yalifunguliwa rasmi tarehe 7 Julai 1980.Kuanzia hapo
makumbusho haya yaliendelea kutoa huduma chini ya usimamizi wa Mkoa wa Ruvuma
na wazee wameendelea kufanya maadhimisho ya kila siku ya mashujaa katika eneo
la Makumbusho haya ila mwaka.
Baadhi ya wazee ndio ambao wamekuwa wakitoa maelezo kwa
wageni wanaotembelea makumbusho haya. Tarehe 1 September 2005 makumbusho haya
yalikabidhiwa kwa Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Miaka 100 ya vita vya Maji
Maji iliadhimishwa kitaifa katika Makumbusho haya tarehe 27 Februari 2006 na
yalizinduliwa rasmi na Rais wa Tanzania Mhe. Jakaya Kikwete
tuzidi kuwakumbuka mashujaa wetu kwa kupigania uhuru wetu mpaka sasa tupo hapa.mungu aziweke roho za mashujaa wetu ameni
ReplyDeleteDaima tuwakumbuke mashujaa wetu waiouawa kwenye vita vya majimaji
ReplyDeleteMashujaa wetu, Bila ninyi hakuna kitu ambacho leo tunajifurahisha nacho. Daima Tutawaenzi.
ReplyDelete