Monday, 26 August 2013

BARAZA LA MICHEZO LA TAIFA BMT LAFANYA MAFUNZO YA WAAMUZI WA MICHEZO KWA WANAFUNZI WA SHULE ZA SEKONDARI NA MSINGI _RUVUMA

Na Mhaiki Andrew, Songea


BARAZA la michezo la Taifa(BMT) kwa kushirikiana na Mashirikisho matatu ya michezo ikiwemo Soka(TFF), riadha(RT) na wavu(TAVA) wataendesha mafunzo ya waamuzi wa michezo hiyo kwa wanafunzi wa Sekondari na shule za msingi mkoani Ruvuma, mafunzo hayo yanatarajia kuanza kufanyika (Jumatatu).


   Akizungumza na mwandishi wa habari hii  jana, Afisa Michezo,Utamaduni na vijana mkoa wa Ruvuma, Hassan Katuli alisema kuwa mafunzo hayo yatafanyika kwa siku nne kwa lengo la kuwapata waamuzi ambao watachezesha mashindano ya UMISSETA na UMISHUMTA kwenye ngazi ya mkoa.


   Alisema mafunzo hayo yatashirikisha wilaya zote sita za mkoa wa Ruvuma na Maofisa Michezo ndio walioachiwa majukumu ya kuraatibu na kuteua washiriki wa kushiriki mafunzo hayo kwa kuteua vijana kutoka shule za msingi na Sekondari katika wilaya zao,wilaya hizo sita kuwa Nyasa, Namtumbo, Tunduru, Mbinga, Songea Manispaa na Songea vijijini.


   Alisema kila wilaya itateua vijana 10 kuhudhuria mafunzo ya soka, 12 watahudhuria mafunzo ya uamuzi wa mpira wa wavu na wanafunzi 13 watapata fursa ya kuhudhuria mafunzo ya uamuzi wa riadha ambayo yataendeshwa kwa vitendo na nadharia na wanafunzi ambao wanaotarajia kumaliza elimu ya msingi na Sekondari hawataruhusiwa kuhudhuria mafunzo hayo.


  Katuli, pia alisema Afisa michezo  hatakaye shindwa kuteua wanafunzi wa kuhudhuria mafunzo hayo kutokana na chuki zake binafsi alidai ofisi ya Mkuu wa mkoa itamchukulia hatua kwa kumwajibisha kwa kufuata misingi ya utumishi wa umma, ili kuweza kudhibiti uzembe ambao unaweza kujitokeza na kuwepo na visingizio vya kushindwa kutekeleza hilo


    Alisema mafunzo hayo ni muhimu kwa wanafunzi kwani yatakuwa yanamjengea uwezo na hamasa ya kupenda michezo kwa kujiendeleza baadaye, punde atakapomaliza elimu ya msingi na Sekondari , badala ya kutegemea kuomba waamuzi kutoka kwenye vyama na kwenda kuchezesha mashindano ya UMISSETA na UMISHUMTA kila mwaka.


MWISHO

No comments:

Post a Comment

TUPE MAONI YAKO