Na Anna Nkinda – Maelezo , Lindi
Mjumbe wa Halmashauri kuu ya Chama
Cha Mapinduzi (CCM) taifa (NEC) Mama Salma Kikwete amewataka wakazi wa
kijiji cha Kitumbikwela na Mingoyo wilayani Lindi mjini kuchangamkia
punguzo la kuingiza umeme katika nyumba zao na kuepukana na gharama za
mafuta ya taa ambazo zinapanda mara kwa mara.
Mama Kikwete ambaye pia ni Mke wa
Rais aliyasema hayo jana wakati akiongea kwa nyakati tofauti na
wananchi hao katika ziara yake ya kichama ya kuwashukuru wanachama wa
CCM kwa kumchagua kuwa mjumbe wa NEC kutoka wilaya ya Lindi mjini.
Alisema kuwa miaka ya nyuma
gharama za kuweka umeme majumbani zilikuwa kubwa na kufikia shilingi
milioni mbili na nusu lakini hivi sasa zimeshuka hadi shilingi laki nne
na arobaini elfu fedha ambazo hata mwananchi wa kawaida anaweza
akajiwekea akiba na kuzipata.
Mama Kikwete alisema, “Kuweka
umeme katika nyumba yako si utajiri kwani gharama za uwekaji zimepungua
ukilinganisha na miaka ya nyuma jambo la muhimu ni nyumba iwe
imeezekwa vizuri na kuwekwa nyaya za kuingiza umeme ndani ya nyumba
(wire ring).
Hata kama hauna hela unaweza
kuweka akiba yako kidogokidogo kila mwaka pale unapouza mazao na baada
ya miaka michache utakuwa umepata fedha yote, nawasihi wananchi wenzangu
hakikisheni kuwa umeme utakapofika kijijini mnautumia kwani wenzenu
wanatamani kuwa na umeme lakini bado haujawafikia”.
Aidha Mama Kikwete pia
aliwashimiza wanawake wajitokeze kwa wingi katika miradi ya kukopa mbuzi
lipa mbuzi na kopa ng’ombe lipa ng’ombe kwani wakipata fedha kidogo
pamoja na za waume zao pato la familia litaongezeka na hivyo kujikwamua
kimaendeleo.
Akiwa katika kijiji cha Mingoyo
aliwasihi wazazi kuwalea vijana wao katika maadili mema na kuwaelekeza
pale ambapo wanapokosea kwani utandawazi unawaharibu vijana wengi na
kujikuta wanajiingiza katika matendo yasiyofaa ikiwa ni pamoja na
utumiaji wa madawa ya kulevya na uvutaji wa bangi.
“Baadhi ya vijana wanaona fahari
kuwa na wapenzi wengi jambo ambalo ni la hatari kwa kuwa unajiandalia
mazingira ya kupata kirahisi maambukizi ya virusi vya Ukimwi na takwimu
zinaonyesha kuwa kwa kila watanzania mia moja sita wanamaambukizi.
Muache tabia hiyo na kufuata vitabu vitakatifu vya dini vinavyosema
kwani ugonjwa huu hauna dawa zaidi ya dawa za kupunguza makali tu”,
alisema Mjumbe huyo wa NEC .
Kwa upande wake diwani wa kata ya
Mingoyo Jamridi Mandowa alisema kuwa tangu Serikali ilipotangaza kuanza
kwa mradi wa kusambaza umeme vijijini, kupunguza gharama za ufungaji wa
umeme majumbani na kusogeza muda wa kupokea maombi wananchi wamejitokeza
kwa wingi kutuma maombi lakini kasi ya usambazaji ni ndogo hawaelewi
tatizo ni kitu gani.
Naye Diwani wa Kata ya Msinjahili
ambaye ni Meya wa Lindi Mjini Frank Magali alisema kuwa kata yake
inamradi wa kopa ng’ombe lipa ng’ombe na kopa mbuzi lipa mbuzi ambapo
kwa upande wa ng’ombe walipata majike nane na dume mmoja na kuwakopesha
wananchi ambao kwa kiasi kikubwa wamenufaika na mradi huo.
Mama Kikwete alifanya mikutano ya
hadhara na kujibu maswali ya wananchi wa kata za Msinjahili, Mingoyo
na Mitandi na kuwakabidhi kadi wanachama wapya wa CCM 37, Umoja wa
vijana 37, Umoja wa Wanawake 92 na Jumuia ya Wazazi 73.
No comments:
Post a Comment