Mheshimiwa Balozi Peter Kallaghe akiwa na mwanamuziki
Freddy Macha aliyetumbuiza shughuli hii na gitaa lake. Picha na Fred Mchaki
Anna Luks na Christine Mhando. Picha ya Urban Pulse
Moja ya ubunifu wa Jacquiline Kibacha uliohamasishwa
na jadi ya Wamasai. Picha ya F. Macha
Jacquiline
Kibacha akipokea tuzo ya mapambo iitwayo “Fashions Finest 2012” mjini
London mwezi Novemba mwaka jana. Picha na Simon Klyne
Jacquiline Kibacha anayetumia jina la Heart 365. Picha na F. Macha
Toka kulia, Mama Balozi- Joyce Kallaghe, Anna Lukindo, Mheshimiwa
Balozi Peter Kallaghe, Christine Mhando, Naibu Balozi Chabaka
Kilumanga na mkewe Irene. Picha na Urban Pulse
Naibu Balozi na mkewe Irene, Aruna Mbeyu, Chichia
London, Balozi P Kallaghe, Anna Luks, Mariam Mungula wa CCM Barking. Picha na Fred Mchaki.
Mshoni Christine Mhando (Chichia London) akiongea
na baadhi ya wageni. Picha na Urban Pulse
Anna Luks, Mama Mhando na Chichia. Picha ya Urban Pulse
Wageni wa Kijapani wakiwa na Chichia anayehamasisha fani ya Khanga. Picha na Aaron Miclat.
Marim Mungula, Baraka Baraka, Anna Luks, Wilkins
Kiondo, Chichia, Samson Soboye. Picha na Fred Mchaki.
Picha za Urban Pulse na F. Mchaki
Maonyesho maarufu ya mavazi –London Fashion Week-
yaliyoanza rasmi Ijumaa iliyopita mjini London yameiweka ramani ya
Tanzania duniani.
Shughuli hii muhimu kiuchumi na kisanaa inayoendelea
juma zima na kuhusisha vituo vya kitamaduni na balozi 27 ina
lengo la kutangaza vipaji vya wabunifu mavazi toka nchi zisizojulikana
uwanja huu mahiri wa kimataifa unaosifika takriban miaka 30 sasa.
“London Fashion Week” ni moja ya
maonyesho manne ulimwenguni yaliyoasisiwa rasmi kutukuza ubunifu,
ufundi na biashara mwaka 1984. Huendeshwa sambamba miji ya New
York, Milan na Paris kila mwezi Februari na Septemba.
Watanzania tulioingia kwa dhamira ya “Swahili
Flavour” (Ladha ya Kiswahili) tumefadhiliwa na Ubalozi wa Tanzania
London ukishirikiana na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB). Watayarishaji
wa shughuli hii ni shirika la kitamaduni na elimu Uingereza- British
Council lenye mahusiano ya kirafiki na nchi 100 duniani.
“Maonyesho
ya mavazi London ni fani ya hali ya juu na kibiashara ambapo waume kwa
wanawake huwa pamoja wakibadilishana mapambo na visaidizi vyake,”
anasema Julian Roberts, mbunifu mavazi wa British Council.
Akiongea rasmi kwenye ufunguzi wa Ijumaa uliokuwa
na vinywaji baridi na muziki wa Kiswahili, mke wa Balozi Uingereza,
Mama Joyce Kallaghe aliwasifu wabunifu mavazi wetu na kuwakabirisha
wageni mbalimbali waliohudhuria “kuzitembelea mbuga nzuri za Kitanzania
kama watafurahishwa na mavazi na ladha yetu ya Kiswahili.”
Wabunifu na washoni hao watatu ni Christine
Mhando ( “Chichia London”), Anna Lukindo ( “Anna Luks”) na
Jacquleine Kibacha (“Heart 365”). Kibacha ambaye pia ni mtunzi wa
mashairi huchanganya desturi za kijadi na kisasa kwa shanga shanga,
manyoya ya ndege na mapambo yaliyotokana na sanaa za Wamasai. Miezi
mitatu iliyopita kazi zake Kibacha zilipata tuzo maarufu la “Fashions
Finest 2012.”
Akifafanua fani yake, Christine “Chichia” Mhando
aliyehitimu chuo cha Usanii cha Kent mwaka 2002 alisema yeye huhamasisha
vazi la Kanga, misemo na maneno ya Kiswahili mathalan “Tongoza”,
“Ala Kumbe!” na “Zungumza” kama wajihi wa kazi hiyo. Anna
Luks aliyefuzu shahada ya mwanzo (BA) chuo cha Middlesex, alieleza azma
yake ni kumwonyesha mwanamke wa Kitanzania alivyo kupitia mitindo kama
“dunia pana” , “kaba roho” na “baibui.” Anna Luks huchanganya
ushonaji wa mikono, kamba kamba na mavazi ya kisasa.
Naibu Balozi, Mheshimiwa Chabaka Kilumanga
alisema maonyesho haya ya kimataifa yatakua nafasi kubwa kwa Tanzania
kujitangaza kibiashara na ni sehemu mahsusi ya fahari ya utamaduni wetu.
Wahusika wengine waliochangia mafanikio ya
shughuli ni Mratibu Ubalozini, Bi Rose Kiondo; Afisa mwangalizi wa
onyesho hilo, Samson Soboye na Meneja wa dhana ya Swahili Flavour,
Mike Puplampu.
Habari zilizopatikana jana zilisema kwamba wabunifu
mavazi wa Kitanzania wametajwa ndani ya kundi la washindi kumi bora.
Ushindi huo unathibitisha dhahiri uwezo wa sanaa na ubunifu wetu ndani
ya hulka ya mavazi ya kimataifa.
Tovuti: www.freddymacha.com
No comments:
Post a Comment