POLISI wawili wa Kituo cha Polisi Oysterbay Dar es Salaam, Koplo Senga Idd (47) na Konstebo Issa Mtama (29) na wenzao saba waliokamatwa na vipande 70 vya meno ya tembo vyenye thamani ya Sh milioni 850, walifikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili. Watu hao walikamatwa katika kizuizi cha Kauzeni, Kata ya Vikumbulu Tarafa ya Chole Kisarawe mkoani Pwani.
Watuhumiwa hao walifikishwa katika Mahakama ya Mkoa wa Pwani, wakiwa chini ya ulinzi mkali wa polisi.
Hata hivyo walibainika kukabiliwa na mashtaka mawili ya kukutwa na nyara za serikali kinyume na sheria na kuhujumu uchumi.
Akisoma mashtaka hayo, Wakili wa Serikali, Cecilia Shelly alidai mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mkoa wa Pwani, Bahati Ndeserua alidai washtakiwa walitenda kosa hilo Julai 28 mwaka huu wilayani Kisarawe.
"Watuhumiwa wanashtakiwa wote kwa pamoja kwa kumiliki nyara za serikali vipande 70 vya meno ya tembo bila kibali cha Mkurugenzi wa Wanyamapori,'' alidai Shelly.
Hakimu Ndeserua alisema washtakiwa hawatakiwi kutoa utetezi wowote katika mahakama hiyo kwa vile kesi hiyo inapaswa kusikilizwa katika Mahakama Kuu.
Alisema pia kuwa mahakama hiyo haina uwezo wa kutoa dhamana kwa washtakiwa hao.
"Washtakiwa nadhani wote mmesikia makosa yenu, hivyo mahakama hii haitaweza kuwapa nafasi ya kujibu lolote kwa sababu mamlaka makubwa ya kesi yapo Mahakama Kuu.
“Hii imetokana na kesi yenu kuwa ya kuhujumu uchumi na kukutwa na nyara za serikali kinyume na sheria,'' alisema Ndeserua.
Wengine waliopandishwa kizimbani ni Hamidu Salumu (35), mkazi wa Yombo njia Panda ambaye alikuwa dereva wa gari lililobeba meno hayo aina ya Toyota Surf.
Prospa Maleto (36) wa Tandika Dar es Salaam, Seif Kadro (35) wa Panga la Mwingereza Kata ya Vikumbulu wilayani Kisarawe, Ramadhani Athumani (45) wa Chanika Dar es Salaam nao walifikishwa kortini.
Wengine ni Musa Ally (35) mkazi wa Kinondoni Studio Dar es Salaam, Said Mdumuka (28) wa Panga la Mwingereza Chole wilayani Kisarawe Mkoa wa Pwani na Amri Bakari (33) wa Charambe Mbagala Dar es Salaam.
Watuhumiwa wote walirudishwa rumande na kesi hiyo itatajwa tena Agosti 14 mwaka huu