"NITAENDELEA KUPAMBANA NA WABISHI WASIOTAKA KUHAMA ILI KUPISHA MIRADI YA UJENZI"...MAGUFULI
WAZIRI wa Ujenzi, Dk. John Magufuli ameapa kupambana kwa kuwabomolea au
kuwakomesha kwa njia nyingine, watu waliogoma kuhama kwa ajili ya
kupisha miradi mbalimbali ya ujenzi inayotekelezwa na wizara yake.
Katika hilo, tayari amekwishatangaza uamuzi mzito wa kuruhusu
kampuni ya ujenzi ya Jaspal Singh, kujenga barabara kwa kiwango cha lami
kwa kuzizunguka nyumba za wakazi waliogoma kuhama na kukimbilia
mahakamani akiamini kuwa wataondolewa kwa kugongwa na malori
yatakayokuwa yakipita baada ya barabara hiyo kukamilika.
Pamoja
na hilo, Dk. Magufuli amesema atazibomoa bila kulipa fidia nyumba za
wananchi nane waliokataa kufanyiwa tathmini ili kupisha mradi wa ujenzi
wa daraja la Kigamboni, endapo hawatabadili msimamo wao huo.
Uamuzi
huo aliutangaza jana baada ya kufanya ziara ya kutembelea miradi
mbalimbali katika Jiji la Dar es Salaam, ambapo alibaini kuwa miradi
mingi inakwamishwa na wananchi wa maeneo husika.
Akiwa katika
mradi wa ujenzi wa barabara ya Kigogo hadi Jangwani yenye kilomita 2.7,
alishangazwa kuona mradi umesimama huku vifaa vikionekana kuwa na kutu
kitendo ambacho kilimlazimisha ahoji.
Mhandisi Mshauri wa mradi
huo, Mussa Ali pamoja na Mkandarasi Jaspal Hungh, walimueleza Magufuli
kwamba kuna wananchi wenye nyumba 16 wamechukua fidia na kufungua kesi
mahakamani kwa kudai kiasi walichopewa ni kidogo.
Aliongeza kuwa kesi hiyo imechukua zaidi ya miaka miwili bila kutolewa hukumu na kusababisha mradi kukwama.
TAMKO LA KIGOGO
Akizungumzia
hilo Magufuli alisema: “Naomba tusiingilie mahakama lakini naagiza
kuanzia leo (jana), anzeni kujenga barabara ya lami kwa kuzizungushia
lami nyumba hizo na kuruhusu gari zipite, nadhani haitapita wiki kabla
hazijagongwa na malori ya mchanga, sitaki kusikia Serikali inadaiwa
fidia ya ucheleweshaji wa mradi.
“Pia naagiza kwamba mbele ya
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki kwamba meneja wa mradi
fungua kesi dhidi ya wananchi hao waliochukua fedha za fidia na kwenda
mahakamani, huo ni wizi.
“Serikali ikishinda kesi ya madai yao ya
fidia ndogo, wao ndio watawajibika kujenga sehemu ya nyumba zao,
hatuwezi kuchezea fedha kwani kuwafidia Sh bilioni 3.8 ambapo mradi
wenyewe unagharimu Sh bilioni 7.6.
“Kuna mazoea yameibuka ya watu
kuchezea Serikali na mahakama, sasa nasema katika miradi ya wizara
yangu nitapambana nao watu wenye kiburi cha kuchezea vyombo hivyo,”
alisema.
DARAJA L A KIGAMBONI
Awali akitembelea eneo la
Kigamboni uliko mradi wa daraja la Kigamboni, Magufuli aliwataka
wananchi nane waliokataa kufanyiwa tathmini ya nyumba zao ili kupisha
mradi huo, kubadili msimamo wao haraka kabla ya Serikali haijazibomoa
nyumba hizo kwa nguvu tena bila kulipwa.
Jumla ya watu 121
walitakiwa kuhama kupisha mradi huo ambapo kati yao 113 walikubali
kufanyiwa tathmini na kulipwa jumla ya Sh bilioni 11.7, lakini nane
walikataa.
“Nasema Serikali ikiamua kufanya ukorofi utakuwa
mkubwa kuliko msimamo wako, sasa nasema hao waliokataa kufidiwa naomba
wasiambulie patupu kabla hatua hazijachukuliwa, wakubali kuchukua kiasi
kitakachothaminiwa haraka, sisi tukija tutabomoa na hatukulipi na mradi
utaendelea.
“Naomba daraja hili likamilike na kukabidhiwa kwa
Rais Jakaya Kikwete Januari 31, 2015 na kulifungua, sitaki kuona
linafunguliwa na rais mwingine ambaye anaweza kusema yeye ndiye
aliyejenga wakati ni uongo, aliyeweka jiwe la msingi ndiye
atakayefungua,” alisema.
Mradi wa daraja la Kigamboni unagharimu
Sh bilioni 214 na kati hizo asilimia 40 zinatolewa na Serikali wakati
Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), unachangia asilimia 60.
Mbali
na hilo, Dk. Magufuli ameagiza kuondolewa haraka wakazi wa eneo la Davis
Corner, Temeke ambao licha ya kulipwa fidia ili kupisha ujenzi wa
barabara ya Jet Corner hadi Temeke, wameshindwa kuhama mpaka sasa na
badala yake kutumia fedha hizo kuendeleza ujenzi na kudai malipo
mengine.
Magufuli alishangazwa kuona wananchi hao ambao wamegoma
hadi sasa wamelipwa fidia Sh 15.8 huku mradi wenyewe ukiwa Sh bilioni 12
na barabara ikiwa haijakamilika.
Mradi wa mabasi ya kasi
Akikagua
mradi wa mabasi yaendayo kasi jijini Dar es Salaam (DARTS), Magufuli
alifurahishwa na kasi pamoja na kiwango cha ujenzi wa mradi huo, ambao
utapunguza msongamano wa magari.
Meneja wa mradi wa Darts, Baraka
Ally alimweleza Dk. Magufuli kwamba mradi unaendelea vizuri na
utakamilika kwa wakati uliopangwa.
Hata hivyo alisema changamoto
kubwa inayoukabili mradi huo ni uvamizi wa wafanyabishara ambao
wamekuwa wakiweka biashara zao barabarani huku wenye teksi na magari
mengine wakiegesha eneo la mradi.
Vile vile alisema kuwa kuna
hatari kubwa ya Jiji la Dar es Salaam kukumbwa na harufu kali kutokana
na wakazi wanaoishi karibu na barabara kujiunganishia kinyemela mabomba
ya maji machafu na mifereji ya mvua.
Magufuli aliagiza watu wote
wanaokwamisha mradi huo kuchukuliwa hatua kali, ikiwa ni pamoja na
halmashauri kuwajibika katika hilo.
No comments:
Post a Comment