Na Eeuteri Mangi na Hussein Makame – Maelezo.
Rais
wa Jamuhuri ya watu wa China Xi Jinping (pichani) anataraija kuanza
ziara ya kihistoria nchini tangu kuapishwa kwake kuitumikia nchi hiyo
ambapo katika ziara hiyo atasaini mikataba 17 ya ushirikiano wa
kiuchumi kati ya Serikali za Tanzania na nchi hiyo.
Akiongea
na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa kimataifa Bernard Membe alisema kuwa ziara hiyo ni ya
kwanza barani Afrika kwa Rais huyo mpya wa China baada ya kuchaguliwa
kuliongoza taifa hilo Machi 14 mwaka huu.
Lengo
la ziara hiyo ambayo itaanza tarehe 24 hadi 25 Machi mwaka huu ni
kukuza uwekezaji na biashara baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya
Watu wa China.
Baadhi
ya Mikataba hiyo itahusiana na uboreshaji wa sekta ya viwanda, kilimo
hasa cha tumbaku ikiwemo kuwatafutia soko wakulima kutoka mikoa ya
Tabora na Ruvuma ili waweze kuuza zao hilo katika soko la China.
Waziri
Membe alisema kuwa; “Mikataba mingine ni ya kulipatia Shirika la
Utangazaji Tanzania zana za kufanyia kazi na kuandaa mazingira ya ujenzi
wa bandari ya Bagamoyo itakayounganishwa na reli ya Tanzania na Zambia
(TAZARA), reli ya kati na barabara”.
Rais
Xi Jinping pia atazindua na kukabidhi rasmi kituo cha Mikutano cha
Kimataifa cha Mwalimu Julius Nyerere chenye ghorofa tatu na kumbi nne
za mikutano zenye uwezo kupokea washiriki zaidi ya 1800 kilichogharimu
dola za kimarekani milioni 29.7 zilizotolewa na Serikali ya China kwa
lengo la kumuenzi Mwalimu Nyerere.
Waziri
huyo alisema kuwa baada ya kufika nchini Rais Xi Jinping atazungumza na
mwenyeji wake Rais Dk. Jakaya Kikwete pamoja na Viongozi Waandamizi wa
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na baadaye atahudhuria dhifa
ya kitaifa Ikulu Jijini Dar es salaam.
Siku
ya pili ya ziara yake Rais Jinping atazungumza rasmi na Rais wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk Ali Mohamed Shein
pamoja na ujumbe wa viongozi waandamizi kutoka Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar.
Waziri
Membe aliongeza kuwa Rais Jinping atatoa hotuba maalumu kwa Tanzania,
Afrika na Dunia kwa ujumla na kuzungumzia sera ya Serikali mpya ya
China kwa bara la Afrika ambayo itahudhuriwa na watu kutoka kada
mbalimbali ikiwemo Viongozi na Maafisa Waandamizi wa Serikali, Wahadhiri
wa Vyuo Vikuu,Wabunge, Viongozi wa Dini na Asasi za Kiraia na Wanafunzi
kutoka vyuo mbalimbali.
“Hotuba
hiyo ya Rais wa China ataitoa kwa lugha ya Kichina na kutafsiriwa kwa
lugha ya Kiingereza na Kiswahili ili iweze kuifika dunia nzima, hivyo
tunaviomba vyombo vya habari nchini vichukue fursa hiyo kuwa vya kwanza
kuutangazia Ulimwengu” alisema Waziri Membe.
Ziara
hiyo ya Rais wa Jamhuri ya Watu wa China ni muendelezo wa uhusiano
mzuri kati ya nchi hiyo na Tanzania ulioasisiwa na viongozi wa mataifa
hayo mawili, yaani Mao Zedong wa China na Mwalimu Julius Nyerere wa
Tanzania.
Rais
Jinping ataondoka nchini Machi 25 saa 10:40 jioni kuelekea nchini
Afrika Kusini kuhudhuria mkutano wa tano wa Wakuu wa Nchi zinazokuwa kwa
kasi kiuchumi ambazo ni Brazil, Urusi, India, China na Afrika ya Kusini
(BRICS).
No comments:
Post a Comment