Tuesday, 2 April 2013

MKASA wa baba kumuua mwanae kwa kumzika akiwa hai kutokana na mgogoro wa ndoa, umezidi kuibua mapya, baada ya mama mzazi wa marehemu ,Debora Riziki (3), kusimulia mkasa mzima .

Marehemu Debora Riziki miaka 3 enzi za uhai wake
Hapa maiti ya mtoto Debora ikiwa imetolewa nnje mara baada ya kufukuliwa ndani ya nyumba ya baba yake mzazi 
Hatimae sasa Debora anazikwa
Mara tu baada ya mazishi baba mzazi wa Debora anapelewa kituo cha polisi Tukuyu
 Mama mzazi wa Marehemu, Esther Mwambenja, alisema kabla ya tukio hilo kutokea kulikuwa na viashiria vingi vya mumewe kufanya ukatili
Bibi wa marehemu Debora 
Tukiwa na baadhi ya waandishi wenzangu tukiendelea kupata historia fupi ya marehemu Debora toka kwa mama yake mzazi
 Novemba 15 mwaka 2012 serikali ya kijiji chini ya Mwenyekiti, Lutengano Mwakyoma na mashahidi watano wakiwemo wazazi na ndugu zake, walinikabidhi barua ya kuridhia kuondoka na mwanangu, huku ikimuonya mume wangu kutorudia kosa hili la kumuiba mtoto hadi hapo atakafikisha miaka saba.
 Dada wa marehemu Debora, Neema Stevini(5) kulia ambaye ni mtoto wa kufikia wa baba mzazi wa marehemu, akisimulia jinsi mdogo wake alivyoibwa , alisema kuwa anakumbuka mara ya mwisho ilikuwa jioni majira ya saa 12 jioni.

“Nilitaka kwenda nao, lakini baba Debora akaniambia nirudi kuchochea moto ndani na niliporudi nikakuta wameondoka na nilipokimbilia sana siku waona” alisema kwa masikitiko Neema.
Mwandishi Mkuu wa Mbeya yetu Joseph Mwaisango akiwaanasindikizwa na dogo Asajile huku akielezwa ni jinsi gani walimfahamu mtoto mwenzao Debora kwakweli watoto hawa wamesema hawaamini kabisa kama Debora hawata mwona tena



MKASA wa baba kumuua mwanae kwa kumzika akiwa hai kutokana na mgogoro wa ndoa, umezidi kuibua mapya, baada ya mama mzazi wa marehemu ,Debora Riziki (3), kusimulia mkasa mzima .

Akizungumza kwa hisia kali, katika mahojiano maalumu  na Mbeya yetu kijijini kwake Ibula, katika kata ya Kiwira, wilayani Rungwe, Mama mzazi wa Marehemu, Esther Mwambenja, alisema kabla ya tukio hilo kutokea kulikuwa na viashiria vingi vya mumewe kufanya ukatili.

Alisema  tukio la mzazi mwenza huyo kumwiba mtoto  na kwenda kumfanyia  ukatili huo wa kinyama lilikuwa la pili, baada ya awali kumuiba akiwa na miaka miwili na miezi mine na alimrudisha kwa maandishi ya serikali ya kijiji.

Alisema katika tukio la kwanza la mtalaka wake huyo kumuiba mtoto wao huyo, lilitokea Septemba mwaka 2012, baada ya wiki chache za kumfukuza katika nyumba waliyokuwa wakiishi katika kitongoji cha Iponjola, kijiji cha Asenga, nyumba iliyotumika kuzikwa mtoto huyo.

Alitaja sababu za yeye kufukuzwa ni ugomvi uliotokana na yeye kuhoji  sababu za kuficha fedha kiasi cha sh. 120,000 zilizotokana na wao  kwa pamoja kufanya  kazi ya kibarua katika mashamba kijijini hapo na baada ya malipo kutolewa mtalaka wake huyo alionesha kiasi kidogo cha sh.80,000.

Alisema ugomvi huo ndio ulisababisha  yeye arudishwe kwa wazazi wake, lakini baada ya muda mfupi mwanaume huyo  alimfuata na kumbembeleza ili warudiane na alipogoma aling’ang’ania aondoke na mtoto .

“Nakumbuka ilikuwa Novemba mwaka jana baada ya mimi kuondoka nyumbani kwake na kurudi kuishi hapa nyumbani, siku hiyo tukiwa shambani huyo bwana alikuja hapa nyumbani na kumkuta mwanangu wa kwanza (Neema Steven ) niliyezaa na mwanaume mwingine” alisema Mwambenja.

Alisema baada ya kufika eneo hilo majira ya saa mbili asubuhi alitumia ujanja na kufanikiwa kumuiba mtoto na kisha kutokomea naye kijijini kwao Asenga, hali ambayo ilisababisha kutoa taarifa kituo cha polisi Kiwira.

“Unajua kuwa baada ya kwenda kutoa taarifa polisi walitusaidia kufika kijijini kwao ambapo serikali ya kijiji ilikubali nimchukue mwanangu kwa kuwekeana mkataba wa kisheria kwa mujibu wa sheria, kwani alikuwa chini ya miaka saba”.

Aliongeza kuwa  Novemba 15 mwaka 2012 serikali ya kijiji chini ya Mwenyekiti, Lutengano Mwakyoma na mashahidi watano wakiwemo wazazi na ndugu zake, walinikabidhi barua ya kuridhia kuondoka na mwanangu, huku ikimuonya mume wangu kutorudia kosa hili la kumuiba mtoto hadi hapo atakafikisha miaka saba.
  
Tukio la pili la kuiba mtoto.

Alisema tukio hilo lilitokea Novemba 29 mwaka jana 2012, ambapo alifika nyumbani kwao majira ya saa 12 :00 na kumkuta dada wa marehemu kumchukua mtoto akimdanga kuwa anaenda kusenya kuni eneo la jirani.

Aliongeza kuwa baada ya kuona dada wa marehemu anang’ang’ania kwenda wote alimuamuru arudi nyumbani kuchochea moto kwa kuwa kulikuwa kumeinjikwa mboga na kukubali kurudi.

“kwa mujibu wa maelezo ya mwanangu huyu wa kwanza alisema baada kurudi toka ndani, alikuta baba yake huyo ameondoka na mtoto na tuliporudi na kupokea taarifa hizo tulichanganyikiwa na kuanza kuhangaika hovyo” alisema mama wa marehemu.

Mwambenja alisema kuwa baada ya kucha siku ya pili asubuhi yake walienda kutoa taarifa kituo cha polisi cha Kiwira ili waweze kupata msaada wa kumtafuta, huku wakionesha barua ya makubaliano ya awali ya yeye kuwa na haki ya kisheria ya kusimamia malezi ya mwanao hadi afikishe miaka saba.

Alisema baada ya kutoa taarifa hizo kituoni hapo, askari aliyekuwa zamu siku hiyo alimtaka kutoa kiasi cha shilingi 50,000 ili fedha hizo wapewe askari mgambo wa kwenda  kijijini kwa mzazi mwenzake huyo, kwani tayari walikuwa na taarifa kuwa alikuwa amekimbilia huko.

 “Kutokana na hali ngumu ya maisha tulikosa kiasi hicho cha fedha  hivyo suala hilo kubaki bila msaada wa  polisi na pia hatukuweza kwenda kwa kijijini kwao”.

Aliongeza “sababu ya mimi kuwa mzito kuendelea kumfuatilia kijijini kwao kwa mara ya pili ili kujua kama yupo huko na mtoto ilitokana na hofu niliyoijenga, kwani awali tukiwa kwenye ugomvi alitamka maneno ya vitisho kuwa endapo nitaendelea kung’ang’ania kumchukua mtoto pale anapomchukua atakuja kumuua ili tukose wote”.

Hata hivyo mama huyo mzazi wa Debora, alisema kuwa baada ya kuona hali hiyo, aliendelea kuwasiliana na wifi yake , Bupe Mwangoka,ambaye ni dada mkubwa wa mume wake  anayeishi eneo la Isanga  Jijini mbeya, ambaye ndiye alisaidia kwa kiasi kikubwa kubainika kwa  unyama aliofanya.
  
Maisha kabla ya tukio.

Akielezea maisha yao kabla ya kutengana na baadae kuamua kufanya ukatili huo, alisema aliwahi kumtamkia maneno makali wakati akiwa na ujauzito wa miezi nane .

Alisema baada ya kuibuka ugomvi katika kipindi hicho, mwanaume huyo alimtaka kwenda kuiuza mimba ile kwa mwanaume mwingine yeyote atakayempenda ili asije akazaa mtoto ambaye atachanganya damu ya koo hizo mbili.

“Maneno yale katika kipindi hicho sikuyatilia maanani kwani nilifikiri zilikuwa ni hasira, lakini leo hii ndio najua maana ya ile kauli ” alisisitiza Mwambenja.

Hata hivyo alisema inashangaza kwani  kuna wakati tukiwa katika maisha ya kawaida kabla ya yeye kufanya tukio hilo, mara kadhaa alijutia na kuonya juu ya matukio machafu yaliyojitokeza na kusikika ya watu kuuawa au kuondolewa baadhi ya viungo vya miili yao.

Aidha, alieleza mkasa mwingine wa mume wake huyo ni ule wa wao kufukuzwa katika mji wa Kiwira walikokuwa wakiishi awali kwa kufanya shughuli za umachinga.

Alisema walitimuliwa na serikali ya mtaa katika mji huo kutokana na mumewe huyo kutuhumiwa kuiba simu ya mkononi ambapo alipokea kipigo kikali na baadae kufukuzwa.

Kutokana na hali hiyo, mama wa marehemu Debora alisema yote yaliyotokea amemwachia mungu na kwamba kama ingekuwa uwezo wake angeamuru naye anyongwe, hivyo mamlaka husika zitajua cha kufanya.

Kwa upande wake dada wa marehemu Debora, Neema Stevini(5) ambaye ni mtoto wa kufikia wa baba mzazi wa marehemu, akisimulia jinsi mdogo wake alivyoibwa , alisema kuwa anakumbaka mara ya mwisho ilikuwa jioni majira ya saa 12 jioni.

“Nilitaka kwenda nao, lakini baba Debora akaniambia nirudi kuchochea moto ndani na niliporudi nikakuta wameondoka na nilipokimbilia sana siku waona” alisema kwa masikitiko Neema.

Hata hivyo uchunguzi wa Mbeya yetu umebaini kuwa marehemu Debora alifariki dunia siku hiyo ya Novemba 29 mwaka jana, majira ya saa nne usiku baada ya baba yake kufanikiwa kumuiba kutoka nyumbani kwa mama yake.

Inadaiwa kuwa baada ya kufanikiwa kumtorosha baba huyo wa marehemu alitembea kwa mguu umbali wa kilomita 50 kutoka kijiji cha Ibula alikomuiba hadi nyumbani kwake kijiji cha Isange katika kata ya Isange.

Imeelezwa kuwa baada ya kufika nyumbani kwake, baba huyo mzazi wa marehemu alichimba shimo katikati ya sebule na kumchukua mtoto wake huyo akiwa usingizini na kisha kumfukia akiwa hai.

“Mwanaume Yule alikuwa katili sana, kwani baada ya kumfukia alichukua meza ya chakula na kuiweka juu yake huku akiipamba kwa magazeti jambo ambalo lilifanya ndugu zake wasigundue kirahisi” alisema mpasha habari.

Chanzo hicho kilisema baada ya kufanya hivyo aliishi kwa wiki moja na baadae kukimbilia Jijini Mbeya ili watu wasibaini juu kitendo alichofanya na kwamba kila alipohojiwa na ndugu zake alisema mwanae huyo alimuweka kwa rafiki yake Jijini Mbeya.

Hata hivyo baada ya danadana za muda mrefu ndipo dada wa mtuhumiwa huyo aliamua kutoa taarifa jeshi la polisi na kufanikiwa kumkamata akiwa katika harakati za kutorokea wilayani Chunya na alipobanwa alifichua siri ya alipo mwanae kwa kueleza kuwa alimuua na kumfukia ndani kwake.

Joseph Mwaisango
Ezekiel Kamanga
na
Venance Matinya

LADY JAY DEE KUFUNGUA KITUO CHAKE CHA REDIO HIVI KARIBU..KAENI MKAO WA KULA

Baada ya kutoa makavu live kwa radio ya watu(people's station)/Clouds fm radio kuwa wana upendeleo kwa kupiga nyimbo za watu wao tu na sio za wasanii wa watu wanaopendwa na watu, ikiwemo wimbo wake mpya wa Joto hasira kutokupigwa katika radio hiyo Lady Jay Dee yupo mbioni kufungua kituo chake cha Radio kitakachoitwa KWANZA FM pengine ili kusaidia wanamuziki wengi hasa wachanga ambao ni shida kusikika hewani mara nyingi hata kama nyimbo zao ni nzuri. Lady Jay Dee jana ali-tweet "Kwanza FM coming soon, Yangu mwenyewee". 

Mwanamuziki huyo anayeheshimika katika nchi za Afrika mashariki na aliyefanikiwa kupitia kazi zake za muziki anaonekana alikuwa anaumizwa na jambo hilo la ubaguzi katika kupita nyimbo za wasanii redioni kwa muda mrefu ila alikuwa anajipanga sawa sawa hivyo kwa sasa yupo tayari kwa vita yeye kama Komandoo Binti Machozi aliandika "Huwezi kuanza mapambano km hujajizatiti, si utapigwa ufe.? Vita ni pale tu unapokuwa tayari. Sikuwa tayari huko nyuma ndio maana sikuongea".

Huyo ndiye Lady Jay Dee a.k.a Komandoo Binti Machozi ambaye kabla ya vita ni lazima ajipange na kujidhatiti vizuri kama tweet zake zinavyojieleza.

Sunday, 31 March 2013

TANZANIA HAINA HISTORIA YA UMWAGAJI WA DAMU KWA RAIA WAKE HATA WAKATI WA KUDAI UHURU WAKE , ILA SASA TUNAONA DALILI ZA UMWAGAJI WA DAMU KWA BAADHI YA RAIA WAKE.

 Askofu Mkuu Dkt Norbert Mtega akibariki waumini baada ya Ibada ya PASAKA Kanisa kuu la Songea leo.
Waumini wakiwa katika Ibada ya PASAKA
 Waumini
 Kwaya ya DONBOSCO ambayo imekoleza ibada hiyo leo siku ya PASAKA
 Zifuatazo ni picha za umoja wa Wanamama Katoliki ( WAWATA) ,Wa Jimbo la Songea
 Kutoa vipaji akina mama ( WAWATA)

 Vipaji akina mama ( WAWATA )
Katika masomo ya Ibada ya PASAKA akina mama wa WAWATA wakipeleka Biblia ili kwenda kusoma na baadaye Injili.Aliyeshika Biblia menye gauni la kijani ni Bi. Cosensa Mbena na wa pili ni Bi Geni.
KATIKA Ibada ya PASAKA kwenye kanisa kuu la  Katholiki la Jimbo kuu la Songea la Mt.Mathias Mulumba Kalemba mjini Songea,ambao waumini wa kanisa hilo waliungana na wenzao Duniani kote kwa sherehe za PASAKA,
Hata hivyo alisema kuwa nchi ya Tanzania haikuwa na Historia ya umwagaji wa damu hata wakati wa kudai Uhuru wake,lakini kuna baadhi ya raia wamemwaga damu kutoka kwa watu wasio eleweka.
 
Hayo yametolewa katika mahubiri ya Askofu Mkuu wa Jimbo hilo,Dkt.Norbert Mtega katika Ibada ya sherehe za PASAKA leo,na kwamba ukombozi wa Yesu Kristu kwa kufa na kufufuka kwake uwe kwa watu wote wanao mwamini Mungu hata kama hawajabatizwa.
Aliwashukuru sana waandishi wa habari katika mchango wao wa kuandika na kuripoti uharibifu na vifo kadhaa vilivyo jitokeza katika nchi yetu na wengine  kupata vilema vya kudumu kama vile kutolewa macho.
 
Alisema kuwa waumini waende kumtangaza ufufuko wake wa  amani,upendo na mshikamano,bila ya kujali tofauti za Imani miongoni mwao,kwani wote ni wana wa Mungu.
Aidha alisema kuwa waumini wanatakiwa kuwa na Biblia mikononi mwao,nyumbani kwao na msalaba ambao ni ukombozi wao,kwani Biblia ni neon la Mungu la uzima ,nasio kama vitabu vingine.na kwamba wanawake wameonekana kuwa na mwamko wa kuwa na Biblia na kushiriki katika Jumuia ndogondogo.

Amewataka wanaume nao kushiriki katika uinjilishaji kwa kwenda kwenye Jumuiya ndogondogo ,pamoja na Biblia kama wanavyo fanya wanawake,ambapo Umoja wa Wanawake katoliki ( WAWATA ) Jimbo la Songea walitoa vipaji katiba Ibada ya PASAKA.
 
Chanzo http://ruralpresssongea.blogspot.com

Friday, 29 March 2013

RAIS KIKWETE AFIKA ENEO LA TUKIO NA KUSHUHUDIA HALI HALISI YA KUANGUKA KWA JENGO LA GHOROFA 16 JIJINI DAR,HALI YA UOKOAJI UNAENDELEA


Rais Jakaya Kikwete akisalimiana na Mbunge,Mh Mbatia muda mfupi mara baada ya kufika na kujionea hali halisi ya jengo la Ghorofa lililoporomoka mapema leo asubuhi na kupelekea watu wawili kupoteza maisha na wengine 17 kujeruhiwa vibaya.,aidha shughuli za ukoaji zinaendelea kwani inadaiwa kuna watu wengi zaidi wamefunikwa na jengo hilo.

Monday, 25 March 2013

MSANII WA FILAMU KAJALA MASANJA AACHILIWA HURU LEO!

Leo ndio siku hukumu ya kesi iliyokuwa ikimkabili muigizaji Kajala iliposomwa.Katika kesi hiyo Kajala alihukumiwa miaka nane jela au kulipa faini ya milioni 13.Hivi ninavyoandika Kajala yupo nje baada ya pesa hizo kutolewa na muigizaji mwenzake Wema Sepetu.
 
Katika kesi hiyo ambayo Kajala hakuwahi kupata dhamana alikuwa ndani muda wote.Machi 15, mwaka jana Kajala na aliyekuwa mumewe walifikishwa mahakamani wakikabiliwa na kosa la utakatishaji fedha haramu ambapo kwa mujibu wa sheria kosa hilo halina dhamana.
 
Washtakiwa hao walikuwakabiliwa na makosa matatu, kosa la kwanza ni la kula njama ambapo washtakiwa wote kwa pamoja walitenda kosa kwa kuhamisha umiliki wa nyumba iliyopo Kunduchi Salasala jijini Dar es Salaam.Shtaka la pili ni ni kwamba Aprili 14 mwaka 2010 waliamisha isivyo halali umiliki wa nyumba hiyo kinyume na kifungu cha 34(2)A(3) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya mwaka 2007. Shitaka la tatu ni la kutakatisha fedha ambalo walilitenda Aprili 14 mwaka 2010 huku wakijua ni kinyume cha sheria.
Kajala pichani walipocheza filamu ya DEVEL KINGDOM ya Kanumba pamoja na Noah Ramsey wa Nigeria.

Habari zaidi kesho katika movie leo na Zamaradi Mketema aliyekuwepo mahakama ya kisutu wakati hukumu hiyo ikisomwa!
Pia hongera Wema Sepetu kwa kumshika mkono msichana mwenzako dada!
 
 

JAMABAZI SUGU LAUWAWA KWA KUPIGWA RISASI KWENYE HARAKATI ZA KUTEKA MAGARI MLIMA NYOKA JIJINI MBEYA

Kamanda wa polisi mkoa wa Mbeya  Diwani akiangalia mwili jambazi lililouwawa na kikosi cha polisi Mbeya
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Diwani Athumani akionyesaha hirizi iliyofungwa katika bunduki aliyokuwa anatumia jambazi huyo kama kinga katika matukio yake 
Hii ndiyo hirizi iliyofungwa katika bunduki aliyokuwa anatumia jamabazi huyo jamani waganga wakienyeji acheni hizo kuwadanganya watu matokeo yake ni kuongeza uhalifu nchini hakika nao tutawashughulikia kwani wamekuwa chanzo cha uhalifu nchini hayo yamesemwa na kamanda Diwani,
  ..............................................................
MTU mmoja ambaye anasadikiwa kuwa ni jambazi ameuawa kwa kupigwa risasi na Askari wa Jeshi la Polisi akiwa kwenye harakati za kuteka magari katika Eneo la Mlima Nyoka Jijini Mbeya baada ya kutokea kwa majibizano ya kurushiana risasi.
 
Jambazi huyo ni miongoni mwa watu waliokuwa wakitafutwa na Jeshi la Polisi Mkoani hapa akituhumiwa kuhusika na mauaji ya Askari Polisi mwenye namba G 68 PC Jafari yaliyotokea  Februari 6, Mwaka huu  katika eneo la Matundasi Wilayani Chunya.
  
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Diwani Athumani amethibitisha kutokea kwa tukio hilo katika Mkutano alioufanya na waandishi wa Habari Ofisini kwake ambapo alisema tukio hilo lilitokea  jana majira ya Saa 10(kumi) Alfajiri usiku wa kuamkia Machi 27, Mwaka huu.
  
Kamanda Diwani alisema kabla ya tukio majambazi wapatao wanne  tayari walikuwa wameweka mawe barabarani kwa nia ya kuteka magari ili wafanye uporaji katika eneo hilo la Mlima Nyoka ambalo limekuwa na matukio kadhaa ya watu kuporwa mali zao.
  
Alisema Jeshi la polisi baada ya kupata habari za kutegwa mawe, askari walifika kwa wakati kwa kuwa polisi walikuwa jirani na eneo hilo na kuweka mtego kwa kuwa majambazi hawakuwa wameonekana kwa wakati ule.
  
Aliongeza kuwa baada ya muda majambazi walipoona taa za gari walijitokeza tayari kushambulia lakini kabla ya hapo polisi walitoa amri ya kujisalimisha kinyume chake wakaanza kupiga risasi ovyo ndipo mashambulizi ya polisi yakafanywa.
  
Diwani alisema katika mapambano hayo alijeruhiwa jambazi mmoja kwa risasi kiunoni na ubavuni kulia na wengine watatu walifanikiwa kutoroka ambapo Marehemu alipowahishwa hospitali kwa matibabu daktari alibaini kuwa amekwisha fariki.
  
Alisema  jambazi huyo alikutwa na silaha moja SMG yenye namba  AB huku namba  nyingine zikiwa zimefutwa na magazine yake ikiwa na risasi ishirini na mbili (22) pamoja na mapanga mawili([2).
  
Aliongeza kuwa baada ya  Marehemu kufanyiwa upekuzi maungoni mwake jambazi huyo alikutwa na kitambulisho cha mkazi chenye namba B.0010453 chenye jina la Emanuel Blasius Mdendemi aliyezaliwa mwaka 1984 eneo la Matamba wilayani Makete Mkoa wa Iringa makazi yake ni Uwemba Mkoani Njombe.
  
“Jambazi huyu amebainika kuwa ni miongoni mwa majambazi waliokuwa kwenye mtandao wa majambazi uliokamatwa hivi karibuni kuhusiana na matukio waliyofanya Mikoa mbalimbali ikiwemo Mbeya,Njombe na Iringa.aidha amebainika kushiriki katika tukio la mauaji ya askari polisi PC Jafari wa kituo cha Mkwajuni – Chunya tarehe 06.02.2013.” Alisema Kamanda Diwani.
  
Aliongeza kuwa  ufuatiliaji wa majambazi waliotoroka unaendelea kufanywa ambapo pia  anatoa wito kwa yeyote mwenye taarifa za wahalifu hao azitoe bila kuchelewa kwa jeshi la polisi ili zifanyiwe kazi.

Pia  amewatahadhalisha majambazi na wahalifu wa makosa yeyote kuachana na uhalifu kwa kuwa ni biashara isiyo na faida badala yake wafanye shughuli halali kupata maendeleo ambazo fursa zake ni nyingi. 
 
Picha na  habari kwa hisani ya mbeyayetu.blogspot.com

Picha za matukio ya Kikao cha Baraza la wafanyakazi kinachoendelea kwenye ukumbi wa baraza la Maaskofu kurasini (TEC)


Waziri wa Kazi na Ajira Mh. Gaundentia Kabaka (Mb) akifungua Baraza la Wafanyakazi wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali Pa Kazi (OSHA), mapema leo 25/03/2013, katika ukumbi wa Baraza la Maaskofu Kurasini (TEC) jijini Dar es Salaam
 
 Baadhi ya Wafanyakazi wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali Pa kazi (OSHA), wakimsikiliza kwa makini Mgeni rasmi Waziri wa Kazi na Ajira Mh. Gaundentia Kabaka (Mb)  wakati wa ufunguzi wa Baraza la wafanyakazi  katika ukumbi wa Baraza la Maaskofu Kurasini (TEC) jijini Dar es Salaam

Washiriki wa Baraza la Wafanyakazi wakiwa katika picha ya pamoja na mgeni rasmi Waziri wa Kazi na Ajira Mh. Gaundentia Kabaka (Mb)

Habari zote na Afisa Uhusiano OSHA

TUPE MAONI YAKO