Mwandishi
Mkuu wa Mbeya yetu Joseph Mwaisango akiwaanasindikizwa na dogo Asajile
huku akielezwa ni jinsi gani walimfahamu mtoto mwenzao Debora kwakweli
watoto hawa wamesema hawaamini kabisa kama Debora hawata mwona tena
MKASA wa baba
kumuua mwanae kwa kumzika akiwa hai kutokana na mgogoro wa ndoa, umezidi kuibua
mapya, baada ya mama mzazi wa marehemu ,Debora Riziki (3), kusimulia mkasa
mzima .
Akizungumza kwa
hisia kali, katika mahojiano maalumu na Mbeya yetu kijijini kwake Ibula,
katika kata ya Kiwira, wilayani Rungwe, Mama mzazi wa Marehemu, Esther
Mwambenja, alisema kabla ya tukio hilo kutokea kulikuwa na viashiria vingi vya
mumewe kufanya ukatili.
Alisema tukio
la mzazi mwenza huyo kumwiba mtoto na kwenda kumfanyia ukatili huo
wa kinyama lilikuwa la pili, baada ya awali kumuiba akiwa na miaka miwili na
miezi mine na alimrudisha kwa maandishi ya serikali ya kijiji.
Alisema katika
tukio la kwanza la mtalaka wake huyo kumuiba mtoto wao huyo, lilitokea Septemba
mwaka 2012, baada ya wiki chache za kumfukuza katika nyumba waliyokuwa wakiishi
katika kitongoji cha Iponjola, kijiji cha Asenga, nyumba iliyotumika kuzikwa
mtoto huyo.
Alitaja sababu za
yeye kufukuzwa ni ugomvi uliotokana na yeye kuhoji sababu za kuficha
fedha kiasi cha sh. 120,000 zilizotokana na wao kwa pamoja kufanya
kazi ya kibarua katika mashamba kijijini hapo na baada ya malipo kutolewa
mtalaka wake huyo alionesha kiasi kidogo cha sh.80,000.
Alisema ugomvi huo
ndio ulisababisha yeye arudishwe kwa wazazi wake, lakini baada ya muda
mfupi mwanaume huyo alimfuata na kumbembeleza ili warudiane na alipogoma
aling’ang’ania aondoke na mtoto .
“Nakumbuka ilikuwa
Novemba mwaka jana baada ya mimi kuondoka nyumbani kwake na kurudi kuishi hapa
nyumbani, siku hiyo tukiwa shambani huyo bwana alikuja hapa nyumbani na kumkuta
mwanangu wa kwanza (Neema Steven ) niliyezaa na mwanaume mwingine” alisema
Mwambenja.
Alisema baada ya
kufika eneo hilo majira ya saa mbili asubuhi alitumia ujanja na kufanikiwa
kumuiba mtoto na kisha kutokomea naye kijijini kwao Asenga, hali ambayo
ilisababisha kutoa taarifa kituo cha polisi Kiwira.
“Unajua kuwa baada
ya kwenda kutoa taarifa polisi walitusaidia kufika kijijini kwao ambapo
serikali ya kijiji ilikubali nimchukue mwanangu kwa kuwekeana mkataba wa
kisheria kwa mujibu wa sheria, kwani alikuwa chini ya miaka saba”.
Aliongeza
kuwa Novemba 15 mwaka 2012 serikali ya kijiji chini ya Mwenyekiti,
Lutengano Mwakyoma na mashahidi watano wakiwemo wazazi na ndugu zake,
walinikabidhi barua ya kuridhia kuondoka na mwanangu, huku ikimuonya mume wangu
kutorudia kosa hili la kumuiba mtoto hadi hapo atakafikisha miaka saba.
Tukio la pili la kuiba mtoto.
Alisema tukio hilo
lilitokea Novemba 29 mwaka jana 2012, ambapo alifika nyumbani kwao majira ya
saa 12 :00 na kumkuta dada wa marehemu kumchukua mtoto akimdanga kuwa anaenda
kusenya kuni eneo la jirani.
Aliongeza kuwa
baada ya kuona dada wa marehemu anang’ang’ania kwenda wote alimuamuru arudi
nyumbani kuchochea moto kwa kuwa kulikuwa kumeinjikwa mboga na kukubali kurudi.
“kwa mujibu wa
maelezo ya mwanangu huyu wa kwanza alisema baada kurudi toka ndani, alikuta
baba yake huyo ameondoka na mtoto na tuliporudi na kupokea taarifa hizo
tulichanganyikiwa na kuanza kuhangaika hovyo” alisema mama wa marehemu.
Mwambenja alisema
kuwa baada ya kucha siku ya pili asubuhi yake walienda kutoa taarifa kituo cha
polisi cha Kiwira ili waweze kupata msaada wa kumtafuta, huku wakionesha barua
ya makubaliano ya awali ya yeye kuwa na haki ya kisheria ya kusimamia malezi ya
mwanao hadi afikishe miaka saba.
Alisema baada ya
kutoa taarifa hizo kituoni hapo, askari aliyekuwa zamu siku hiyo alimtaka kutoa
kiasi cha shilingi 50,000 ili fedha hizo wapewe askari mgambo wa kwenda
kijijini kwa mzazi mwenzake huyo, kwani tayari walikuwa na taarifa kuwa alikuwa
amekimbilia huko.
“Kutokana na
hali ngumu ya maisha tulikosa kiasi hicho cha fedha hivyo suala hilo
kubaki bila msaada wa polisi na pia hatukuweza kwenda kwa kijijini kwao”.
Aliongeza “sababu
ya mimi kuwa mzito kuendelea kumfuatilia kijijini kwao kwa mara ya pili ili
kujua kama yupo huko na mtoto ilitokana na hofu niliyoijenga, kwani awali
tukiwa kwenye ugomvi alitamka maneno ya vitisho kuwa endapo nitaendelea
kung’ang’ania kumchukua mtoto pale anapomchukua atakuja kumuua ili tukose
wote”.
Hata hivyo mama
huyo mzazi wa Debora, alisema kuwa baada ya kuona hali hiyo, aliendelea
kuwasiliana na wifi yake , Bupe Mwangoka,ambaye ni dada mkubwa wa mume wake
anayeishi eneo la Isanga Jijini mbeya, ambaye ndiye alisaidia kwa
kiasi kikubwa kubainika kwa unyama aliofanya.
Maisha kabla ya tukio.
Akielezea maisha
yao kabla ya kutengana na baadae kuamua kufanya ukatili huo, alisema aliwahi
kumtamkia maneno makali wakati akiwa na ujauzito wa miezi nane .
Alisema baada ya
kuibuka ugomvi katika kipindi hicho, mwanaume huyo alimtaka kwenda kuiuza mimba
ile kwa mwanaume mwingine yeyote atakayempenda ili asije akazaa mtoto ambaye
atachanganya damu ya koo hizo mbili.
“Maneno yale katika
kipindi hicho sikuyatilia maanani kwani nilifikiri zilikuwa ni hasira, lakini
leo hii ndio najua maana ya ile kauli ” alisisitiza Mwambenja.
Hata hivyo alisema
inashangaza kwani kuna wakati tukiwa katika maisha ya kawaida kabla ya
yeye kufanya tukio hilo, mara kadhaa alijutia na kuonya juu ya matukio machafu
yaliyojitokeza na kusikika ya watu kuuawa au kuondolewa baadhi ya viungo vya
miili yao.
Aidha, alieleza mkasa
mwingine wa mume wake huyo ni ule wa wao kufukuzwa katika mji wa Kiwira
walikokuwa wakiishi awali kwa kufanya shughuli za umachinga.
Alisema
walitimuliwa na serikali ya mtaa katika mji huo kutokana na mumewe huyo
kutuhumiwa kuiba simu ya mkononi ambapo alipokea kipigo kikali na baadae
kufukuzwa.
Kutokana na hali
hiyo, mama wa marehemu Debora alisema yote yaliyotokea amemwachia mungu na
kwamba kama ingekuwa uwezo wake angeamuru naye anyongwe, hivyo mamlaka husika
zitajua cha kufanya.
Kwa upande wake
dada wa marehemu Debora, Neema Stevini(5) ambaye ni mtoto wa kufikia wa baba
mzazi wa marehemu, akisimulia jinsi mdogo wake alivyoibwa , alisema kuwa
anakumbaka mara ya mwisho ilikuwa jioni majira ya saa 12 jioni.
“Nilitaka kwenda
nao, lakini baba Debora akaniambia nirudi kuchochea moto ndani na niliporudi
nikakuta wameondoka na nilipokimbilia sana siku waona” alisema kwa masikitiko
Neema.
Hata hivyo
uchunguzi wa Mbeya yetu umebaini kuwa marehemu Debora alifariki dunia siku hiyo
ya Novemba 29 mwaka jana, majira ya saa nne usiku baada ya baba yake kufanikiwa
kumuiba kutoka nyumbani kwa mama yake.
Inadaiwa kuwa baada
ya kufanikiwa kumtorosha baba huyo wa marehemu alitembea kwa mguu umbali wa
kilomita 50 kutoka kijiji cha Ibula alikomuiba hadi nyumbani kwake kijiji cha
Isange katika kata ya Isange.
Imeelezwa kuwa
baada ya kufika nyumbani kwake, baba huyo mzazi wa marehemu alichimba shimo
katikati ya sebule na kumchukua mtoto wake huyo akiwa usingizini na kisha
kumfukia akiwa hai.
“Mwanaume Yule
alikuwa katili sana, kwani baada ya kumfukia alichukua meza ya chakula na
kuiweka juu yake huku akiipamba kwa magazeti jambo ambalo lilifanya ndugu zake
wasigundue kirahisi” alisema mpasha habari.
Chanzo hicho
kilisema baada ya kufanya hivyo aliishi kwa wiki moja na baadae kukimbilia
Jijini Mbeya ili watu wasibaini juu kitendo alichofanya na kwamba kila
alipohojiwa na ndugu zake alisema mwanae huyo alimuweka kwa rafiki yake Jijini
Mbeya.
Hata hivyo baada ya
danadana za muda mrefu ndipo dada wa mtuhumiwa huyo aliamua kutoa taarifa jeshi
la polisi na kufanikiwa kumkamata akiwa katika harakati za kutorokea wilayani
Chunya na alipobanwa alifichua siri ya alipo mwanae kwa kueleza kuwa alimuua na
kumfukia ndani kwake.
Joseph Mwaisango
Ezekiel Kamanga
na
Venance Matinya
|
No comments:
Post a Comment