Sunday, 23 June 2013

MWENYEKITI UVCCM TAIFA: SIAFIKI SERIKALI MFUMO WA SERIKALI TATU


Sunday, June 23, 2013

MWENYEKITI UVCCM TAIFA
 
ARUSHA, Tanzania

MWENYEKITI wa Umoja wa vijana wa chama cha mapinduzi Taifa (UVCCM), Sadifa Juma Hamisi, amepinga vikali kuwepo kwa mfumo wa serikali tatu kama inavyopendekezwa katika rasimu ya katiba.

Sadifa ameyasema hayo wakati akizungumza na wanachama wasomi wa UVCCM kutoka katika vyuo vikuu mkoani kilimanjaro katika hafla ya kuwaaga wasomi hao na ambapo pia ametunuku vyeti vya uanachama kwa wanafunzi 312 pamoja na kuwakabidhi kadi za uanachama wanachama wapya.


Mwenyekiti huyo ambaye pia ni mbunge wa jimbo la Donge (CCM) zanzibar, amesema uwepo mfumo wa serikali tatu ni mzigo mkubwa kwani kutokana na uduni wa uchumi wan chi yetu itakuwa vigumu kuendesha serikali tatu kwa maana ya serikali ya Zanzibar, serikali ya Tanzania bara na ule wa muungano.

“Jamani tusidanganyane, kuendesha serikali tatu ni mzigo, kwa uduni wa uchumi wetu sidhani kama itakuwa rahisi kuendesha serikali tatu, kama kutakuwa na serikali tatu kuna hatari ya kuvunjika kwa muungano wetu huu maana uwezo kuchangia hatuna, tutajiingiza kwenye matatizo makubwa, vijana tuwe makini na tutumie taaluma zetu kuhimiza umuhimu wa kuwepo kwa muungano huu wa sasa,"

Aidha Sadifa amewahimiza vijana kuwa mfano mzuri kwa jamii huku akiwahimiza kuwa waadilifu, wazalendo, kujiamini na kuwa na nidhamu hali ambayo itasaidia kuwepo kwa amani na usalama wa nchi.


Amesema bila amani na muungano wa wananchi maendeleo hayawezi kupatikana katika nchi ambpo aliwataka vijana kuwa mtari wa mbele kuwaelimisha wananchi wa kawaida juu ya umuhimu wa kuenzi, kudumisha na kuimarisha muungano wa zanzibar na Tanganyika  kama njia pekee ya kuhakikisha nchi inakuwa na amani siku zote.

“Vijana tuna wajibu kubwa wa kuwaenzi waliotuletea muungano wetu wa sasa, taaluma zetu ziwe dira ya jamii katika kuenzi, kudumisha na kuimarisha muungano wetu kwani ndio njia pekee ya kusaidia kudumisha amani na usalama wan chi yetu, tuepuke kujiingiza katika mkumbo wa wale wanaodai nchi haitatawalika,” amesema



Hata hivyo Sadifa amewataka vijana kutodanganyika na vyama vinavyoeneza chuki na maandamano yasiyokuwa na msingi wowote huku akifafanua kuwa kisheria kuandamana na haki ya msingi lakini ifuate sheria na yassingilie haki za wengine.

“Chama pekee katika nchi hii ni CCM, kuna vyama vingine vimeanzishwa ambavyo mimi binafsi naviita ‘Saccos’, hauwezi ukajikopesha fedha kienyejienyeji kama alivyofanya Dk. Slaa! Vijana tuwe makini na saccos hizi ambazo ajenda zao ni kukopeshana na vurugu tu,” amesema Sadifa


Kwa upande wake mwenyekiti wa shirikisho la wanafunzi wa vyuo vikuu wanachama wa CCM kilimanjaro, Wakati Mtulya akizungumzia changamoto wanazokumbana nazo, alisema kumekuwa na urasimu ndani ya bodi ya mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu, ambapo mikopo imekuwa ikitolewa kwa watu wasiostahili huku walengwa wakiendelea kutaabika.
Amesema kuwa kumekuwa na mchezo ndani ya bodi hiyo, ambapo mikopo imekuwa ikitolewa kwa watoto wa matajiri huku wastahili ‘watoto wa wakulima’ wakibaki kuzungushwa na kuwekewa masharti magumu ya kupata mikopo hiyo jambo ambalo limekuwa likichangia kuwepo kwa vitendo vibaya miongoni mwa wanafunzi hao.

“Mikopo ni yetu, sio ruzuku, lazima tukopeshwe kwa wakati kwani lazima tutairudisha lakini jambo la kusikitisha, bodi hii imekuwa ikitoa mikopo kwa watoto wa masaki, huku sisi watoto wea mkulima tukiendelea kuzungushwa na kuwekewa masharti magumu ili kupata mikopo hiyo, hili ni tatizo,” amesema Mtulya (habari na TAIFA LETU.com).

No comments:

Post a Comment

TUPE MAONI YAKO