Waziri
wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dk. Fenella Mukangara (kulia)
akimsikiliza Mwenyekiti wa kikundi cha Nyakalalo kililopo kijiji cha
Kitigiri wilayani Geita, Gideon Msabila (kushoto) ambaye alimuelezea
jinsi walivyonufaidika na mkopo wa mfuko wa maendeleo ya vijana fedha
ambazo zimewawezesha kufungua duka la rejareja la bidhaa za nyumbani.
Waziri
wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dk. Fenella Mukangara (kulia)
akiangalia nguo zinazoshonwa na kikundi cha ushonaji kilichopo kijiji
cha Bugalama wilayani Geita ambacho kimenufaika na mkopo wa shilingi
milioni mbili kutoka mfuko wa maendeleo wa halmashauri hiyo. Waziri Dk.
Mukangara alitembelea kijiji hicho jana ili kuona fedha za mkopo
zimewasaidiaje vijana kujikwamua kimaisha.
Vijana
wa kikundi cha kusaidiana kulima cha Busaka katika kijiji cha Kitigiri
wakifurahia fedha shilingi 50,000/= walizopewa na Waziri wa Habari,
Vijana, Utamaduni na Michezo Dk. Fenella Mukangara (wanne kulia) kwa
ajili ya kununulia soda za sikukuu ya Krismasi . Waziri Dk. Mukangara
aliwahimiza vijana hao kujiunga kwenye vikundi vya maendeleo vya kilimo
ili weweze kupata mkopo wa kununulia pembejeo na kuweza kuzalisha
chakula kwa wingi zaidi.
Waziri
wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dk. Fenella Mukangara (wanne
kulia) akiongea na vijana wa kikundi cha kusaidiana kulima cha Busaka
kilichopo kijiji cha Kitigiri wilayani Geita umuhimu wa kujiunga kwenye
vikundi vya maendeleo vya kilimo ili weweze kupata mkopo wa kununulia
pembejeo na kuweza kuzalisha chakula kwa wingi zaidi .
Waziri
wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dk. Fenella Mukangara (kulia)
akimsikiliza Mwenyekiti wa kikundi cha Bodaboda kilichopo kijiji cha
Bugalama wilayani Geita, Enos Komanya wakati alipotembelea kikundi
hicho ambacho kilipata mkopo kutoka mfuko wa maendeleo wa halmashauri.
Waziri Dk. Mukangara alitembelea kijiji hicho jana ili kuona fedha za
mkopo zilizotolewa na mfuko wa maendeleo ya vijana zimewasaidiaje vijana
kujikwamua kimaisha.
Waziri
wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dk. Fenella Mukangara (wanne
kulia) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa wilaya ya Geita,
Kata ya Bukondo na kijiji cha Kitigiri mara baada ya kumaliza ziara
yake katika kijiji hicho ili kuona fedha za mkopo za mfuko wa maendeleo
ya vijana zimewasaidiaje vijana kujikwamua kiuchumi.(Picha na Anna
Nkinda – Maelezo).
Na Anna Nkinda – Maelezo, Geita
Vijana
wametakiwa kushiriki katika suala la ulinzi na usalama wa maeneo
wanayoishi kwa kujiunga na vikundi vya ulinzi shirikishi ili kulinda na
kusimamia rasilimali za vijiji vyao.
Hilo
litafanikiwa endapo vijana watakuwa na moyo wa kujituma na kutambua
kuwa wanajukumu la kujenga taifa kwa kuhakikisha kuwa wanajiletea
maendeleo yao na nchi kwa ujumla kutokana na kazi mbalimbali
wanazozifanya.
Rai
hiyo imetolewa mjini hapa jana na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni
na Michezo Dk. Fenella Mukangara wakati akiongea kwa nyakati tofauti
na wanavikijiji vya Bugalama na Kitigiri vilivyopo wilayani Geita
alipozitembelea baadhi ya Vyama vya Kuweka Akiba na Kukopa (SACCOS)
zilizopata mkopo kupitia mfuko wa maendeleo wa vijana na fedha za
maendeleo ya mfuko wa Halmashauri.
Dk.
Mukangara alisema kuwa maendeleo ya nchi yanawategemea vijana ambao
ndiyo nguzo ya taifa hivyo basi wizara yake kupitia halmashauri za
wilaya itahakikisha kuwa inatoa mafunzo ya kuwajengea uwezo vijana jambo
la muhimu ni kujiunga katika vikundi vya maendeleo ili waweze kufikiwa
kwa urahisi.
“Uongozi
wa kijiji uhakikishe kuwa unawahimiza vijana na kuwajengea uwezo
katika mtazamo wa kujitengemea, kujituma na kufanya kazi na kujiunga
kwenye vikundi vya maendeleo ili iwe rahisi kupata mkopo kupitia SACCOS
zilizopo vijijini mwenu” alisema Dk. Mukangara.
Aliwataka
wanakijiji hao kuwasimamia vijana wao ili wanawajibike na kutambua
kuwa wanajukumu kubwa la kuhakikisha kuwa wanashiriki katika shughuli
za kilimo cha chakula na biashara jambo ambalo litasababisha kuwa na
chakula cha kutosha na kuepukana na janga la njaa.
Dk.
Mkangara alisema, “Najua nyinyi ni wakulima wazuri ila mnatakiwa
kuboresha kilimo chenu ili muweze kuzalisha mazao mengi na ya ziada ,
vijana wenu washiriki katika kilimo hasa cha mazao ya biashara na siyo
kuwaachia wazee peke yao, wawe tayari kujituma na kuhakikisha kuwa
chakula wanachokula wamekitolea jasho kwa namna moja au nyingine”.
Naye
Mwenyekiti wa Kikundi cha Bucha la nyama ya ng’ombe ambacho kilipata
mkopo wa shilingi milioni mbili kutoka SACCOS ya Bugalama Mathias Lucas
alisema kuwa mkopo walioupata umewawezesha kupanuka kwa biashara na
mtaji, kuongezeka kwa wanachama kutoka wanne hadi kumi na kujenga bucha
kubwa la kuuzia nyama.
“Mkopo
tulioupata umetusaidia kujikwamu kiuchumi na kuweza kukabiliana na hali
ngumu ya maisha , tumeweza kuwaajiri na vijana wengine ambao hawakuwa
na ajira lakini tunakabiliwa na changamoto ya kutokuwa na mtaji wa
kutosha na kufungwa kwa mnada wa ng’ombe wilayani Geita .
Tunaiomba
Serikali iweze kutuongezea fedha ya mtaji kwa kutupatia mkopo mkubwa
zaidi na tupewe mafunzo ya ujasiriamali ili tuweze e kujua umuhimu wa
kuweka akiba na kukopa”, alisema Lucas .
Akisoma
taarifa ya kikundi cha Tupendane ambacho kilipata mkopo wa shilingi
1,400,000/= kutoka SACCOS ya Vijana Bukondo na kujishughulisha na kazi
za ushonaji wa nguo za kike mwenyekiti wa kikundi hicho Meshaka Philipo
alisema kuwa wamefanikiwa kuajiri mafundi cherehani vijana watatu na
kuuza nguo kwa wanakijiji na hivyo kupata fedha za kuinua mtaji wao.
Philipo
alizitaja changamoto zinazowakabili kuwa ni pamoja na mtaji mdogo,
elimu duni ya utunzaji wa kumbukumbu za fedha na ujasiliamali, upungufu
wa vitendea kazi kwa ajili ya ushonaji na usafiri ambao ni baiskeli kwa
ajili ya kupeleka nguo kwenye masoko ya nje ya kijiji.
Katika
kijiji cha Bugalama waziri Dk. Mukangara alitembelea vikundi vya Bucha,
Bodaboda na ushonaji ambavyo vilipata mkopo kutoka SACCOS ya kijiji
hicho kutipia mkopo wa halmashauri ya wilaya ya Geita wa shilingi
milioni tano na katika kijiji cha Kitigiri alikagua vikundi vya
Tupendane na Nyakalalo ambavyo vilipata mkopo kutoka SACCOS ya Vijana
Bukondo ambayo ilipata shilingi milioni tano kupitia mfuko wa maendeleo
ya vijana.
No comments:
Post a Comment