Thursday 5 February 2015

SERIKALI KUDHIBITI UJANGILI WA BIASHARA HARAMU MAZAO YA MALIASILI

mgi
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mahmoud Mgimwa akijibu swali bungeni.
……………………………………………………………………………………
Na Lorietha Laurence-Maelezo,Dodoma SERIKALI imejidhatiti katika kudhibiti ujangili na biashara haramu ya mazao ya maliasili kwa kuridhia na kutekeleza mikataba minne ya kudhibiti ujangali wa tembo na unaovuka mipaka na kulinda mapori ya akiba.


Hayo yalisemwa na Naibu Waziri wa Utalii na Maliasili Mahmoud Mgimwa, bungeni Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mch. Peter Msigwa Mbunge wa Iringa Mjini kuhusu utekelezaji wa maazimio ya kimataifa kukomesha ujangili nchini.

Alisema Tanzania imeridhia na kutekeleza mkataba wa kudhibiti ujangili na biashara ya wanyama walioko hatarini kutoweka kama tembo (CITES) kuhifadhi na kulinda maeneo ya Urithi wa dunia kama pori la akiba la Selous(UNESCO), kudhibiti ujangili unaovuka mipaka (INTERPOL na LATF).

Naibu Waziri Mgimwa alisema katika kutekeleza maazimio hayo serikali iliandaa mikutano miwili ya kimataifa ya uhifadhi iliyofanyika mwezi Mei jijini Arusha na Dar es Salaam kwa kushirikisha wadau wa maendeleo na mashirika ya kimataifa .

“Maazimio ya kikao cha mjini Arusha, Tanzania iliridhia makubaliano maalum ya kikanda kudhibiti uhalifu dhidi ya wanyama pori na ujangili unaovuka mipaka ya nchi za Burundi, Kenya, Malawi, Msumbiji, Uganda, Zambia na Sudani Kusini”alisema Mgimwa.

Aliongeza kuwa Serikali ilizindua mkakati wa kitaifa wa uzuiaji ujangili na biashara haramu ya wanyamapori pamoja na mfuko wa pamoja (Basket Fund) kukabiliana na ujangili. Vilevile Tanzania imefanikiwa kupata faida mbalimbali kwa kutekeleza maazimio hayo ikiwa ni Euro 30,000 na USD 100,000 zilitolewa na UNDP, vifaa mbalimbali vya doria ikiwemo magari 21, helicopter, mahema ,binocular na sare pamoja na kuwajengea uwezo watumishi 100 kwa kuwapatia mafunzo ya kudhibiti ujangiri.

Hata hivyo alisema inaendelea kujenga uwezo wa rasilimali watu, fedha na vitendea kazi katika ukusanyaji na utumaji wa taarifa za kiintelijensia kwa kushirikiana na wananchi pamoja na Taasisi za ndani na nje ya nchi katika kudhibiti ujangili unaovuka mipaka.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAONI YAKO