Thursday 17 January 2013

JIMBO KUU KATOLIKI LA SONGEA LAFUNGA MCHAKATO WA KUMTANGAZA SISTA BERNADETA MBAWALA KUWA MWENYEHERI

 Hili ni sanduku lililowekwa masalia ya Mtumishi wa Mungu  Sista Bernadeta Mbawala katika kanisa la jimbo kuu katoliki la Songea Mkoani Ruvuma ambaye 14.1.2013 jimbo lilifunga mchakato wa kumtangaza mwenyeheri kwa kuadhimisha misa takatifu na kusafirsha taarifa zake zilizokusanywa na mahakama ya mchakato.
 Askofu mkuu wa jimbo kuu katoliki Mhashamu Norbert Mtega akitoa wito kwa watanzania kuchangia mchakto wa kumtangaza sista Bernadeta kuwa Mwenyeheri. na baadaye mtakatifu.


 Maandamano yakielekea ndani ya kanisa kwa ajili ya kuadhimisha misa ya mchakato huo.

Masista wakiwa wameshika picha ya sista Bernadeta Mbawala 
 Masista wakiimba katika misa takatifu ya mchakato huo.
 Hao ni mapadre wa kanisa katoliki la Songea wakiwa ndani ya kanisa 

 Hili ni sanduku lililowekwa masalia ya Mtumishi wa Mungu sista Bernadeta Mbawala.

Jimbo kuu katoliki  la Songea leo limeadhimisha misa takatifu ya kufunga mchakato wa kumtangaza  sista BERNADETA MBAWALA OSB  kuwa mwenye heri na baadaye mtakatifu katika ngazi ya jimbo.
****************************
Akizungumza na waumini wa jimbo katoliki la Songea  Askofu mkuu wa jimbo la Songea  Mhashamu NORBERT MTEGA alisema jimbo kwa upande wake tayari limeshafanya utafiti na kukusanya   taarifa mabalimbali alizoziandika sista Bernadelta Mbawala, ambapo wamepata barua alizoandika enzi za uhai wake zaidi ya mia moja, na machapisho mbalimbali ya magazeti.

Pia walipata sala alizotunga mwenyewe na kuzitumia kusali lakini kazi kubwa ilikuwa ni kuhoji watu kadiri ya sheria za kanisa ambapo tayari wamehoji watu 83, wakiwemo mapadre na watawa kutoka Songea na njombe.

Askofu Mtega aliongeza kuwa kanisa sasa limechukua hatua ya  kuanza  kutafiti na kuzungumza hadharani  ili sista Bernadeta OSB aweze kupata heshima ya kutangazwa mtakatifu.

Askofu huyo wajimbo kuu katoliki la Songea Mhashamu Norbert Mtega katika Mahubiri yake hayo alisema kama sista BERNADETA OSB atafanikiwa kutangazwa kuwa mtakatifu atakuwa ni mtanzania wa kwanza kufikia hatua hiyo, na kuwaomba waumini waendelee kuomba ili mchakato huo ufanikiwe.

Alisema baada ya kumaliza mchakato huo wa ngazi ya jimbo kinachosubiliwa sasa ni kutokea kwa miujiza miwili  na miujiza hiyo itokee popote duniani, ukitokea muujiza kwanza basi sista Bernaderta  atatangazwa kuwa mwenye heri na ukitokea muujiza wa pili atatangazwa kuwa mtakatifu.

Askofu alitumia nafasi hiyo kuwaomba watanzania kuchangia kwa hali na mali zoezi hili la mchakato kwa kuwa kunahitajika zaidi ya dola 20,000/= ili uweze kukamilika.

Aidha Askofu Mtega alimuelezea Sista Bernadeta OSB  Kuwa alizaliwa mnamo mwaka 27/10/1911  katika kijiji cha likuyufisi wakati huo kwa sasa ni manispaa ya Songea, wazazi wake ni Stefan Msikazonge na Agata Mayanda, alibatizwa 5/11/1911 peramiho, kipaimara alipata tarehe 8.12.1921 peramiho, na alijiunga na utawa 7.08.1929 peramiho, Nadhiri za kwanza alipata 11.11.1934  wakati huo hakukuwa na nadhiri za daima na alikufa ta29.11.1950.

Sista Bernadeta Mbawala OSB  kutoka nyumba ya mtakatifu Agnes ya chipole  maisha yake na wazazi wake yalikuwa ni ya sala na kuabudu sana na alikuwa anatokewa na moyo mtakatifu wa yesu n aalikuwa anazungumza sana na bikira maria na mtakatifu Agnes,

Aliugua sana lakini aliunganisha mateso yake nay a yesu kristu na hakuwahi kutamka kutafuta dawa za mitishamba, alitolea mateso yake kwa kuwaombea wakosefu na hivyo amewafundisha wakristu kuyapokea mateso kwa imani kwa kuwa mateso ni moja ya sala na sadaka.

Baada ya kufa kwake miaka 61 baadaye  kanisa limeshuhudia watu wakienda kusali katika kaburi lake na kufanikiwa mambo yao huku hakuna kiongozii wa dini aliyeagiza watu wafanye hivyo huo ni ushuhuda kuwa sista BERNADETA anafaa kuwa mtakatifu.

Kazi kubwa imefanywa na mahakama ya mchakato huo ya kuandaa taarifa za sista Bernadeta ambazo taarifa hizo zimekamilika na Askofu mtega ametia saini na kugonga muhuri tayari kwa kusafirishwa kwenda ROMA  kwa mchakato zaidi.

Naye padre CAMILIUS HAULE  naibu wa askofu aliyemwakilisha  askofu katika kufanya kazi kwenye Mahakama ya mchakato  huo  akiwa ni mtetezi wa haki  ametoa tamko .nanukuu  hakuna kitu chochote cha kutiliwa shaka kati ya yale yote yaliyokusanywa na mahakama ya mchakato na ndio yatamkwe hivyo.

Kwa upande wake waziri wan chi ofisi ya makamu wa Rais mazingira  dokta terezya huvisa ametoa ushuhuda mbele ya waumini kuwa amekuwa akiomba katika kaburi la sista Bernadeta na kupata mafanikio ikiwa pamoja na uongozi na ametoa mchango wa shilingi milioni mbili kwa ajili ya mchakto na ujenzi wa kanisa la lizaboni katika manispaa ya songea.

Taarifa za sista bernadeta ndio zinazosafirishwa kwenda ROMA kwa ajili ya kuendelea na mchakato zaidi lakini Masalia ya mwili wake yamebaki katika sanduku la mbao katika kanisa la jimbo kuu katoliki  la songea kwa wale wote wanaohitaji kusali katika masalia hayo wanaalikwa.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAONI YAKO