Thursday 12 September 2013

KINANA- SERIKALI TATU TANZANIA ITASHANGAZA DUNIA.

 
Aonya zitasababisha machafuko 
 

Asema Tanzania itashangaza dunia
   

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimeendeleza msimamo wake wa kupinga muundo wa Serikali tatu kuingizwa katika Katiba mpya, kikisema kuwa muundo huo ni hatari kwa umoja na mshikamano wa taifa.
Chama hicho kimeonya kuhusu muundo huo na kusema kuwa Serikali zaidi ya mbili zinaweza kuvuruga ustawi wa taifa, kwani ni rahisi zaidi nchi kuingia katika machafuko.
Tamko hilo lilitolewa jana na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, alipokuwa akihutubia mamia ya wananchi katika Wilaya ya Shinyanga Vijijini.

Kinana alisema muundo wa Serikali tatu ni mzigo kwa taifa na kwamba Tanzania itakuwa nchi ya kwanza kuwa na marais watatu, jambo ambalo halipo duniani kote. 
“Katiba ni jambo muhimu kwa ustawi wa nchi yetu, lakini katika hili la kuwa na Serikali tatu ni hatari, kwani kwa mujibu wa rasimu yetu ya sasa, inaonyesha kuwa kila Serikali itakuwa na mamlaka kamili.
“Ikiwa kutatokea serikali moja kati ya hizo tatu na moja ikasema sasa inanunua vifaa vya kujilinda, basi ile ya Zanzibar nayo itafanya hivyo na ile ya Muungano pia itafanya hivyo.
“Hata kama kuna vita serikali moja ikasema hatutaki nyingine itasema tunataka, mwishowe mtaanza kupigana wenyewe kwa wenyewe,” alisema Kinana na kuendelea: 
“Kwa hali hiyo, ninachotaka kuwaambia ni kuwa Katiba Mpya itaandikwa na maisha yale yale yataendelea. Afrika Kusini, India na Kenya wamebadili katiba zao, lakini hali ya maisha ya wananchi wao iko vilevile,” alisema.
Katika mkutano huo, Kinana alisema msimamo wa chama chake kuhusu muundo ni Serikali mbili na kueleza kuwa chama chake kitaheshimu maoni ya Watanzania kuhusu muundo wowote bila shinikizo la kisiasa.
Alisema hatua ya kuwa na wingi wa Serikali kuna hatari ya nchi kuwa na Bunge la Mabwenyenye na Bunge la Makabwela, ambapo alisema kuna hatari ya fedha za walipa kodi kutumika vibaya.
Kinana alionya hatua ya kuwa na ukubwa wa Serikali ambayo itakuwa mzigo kwa Watanzania, ambao wamekuwa wakiendesha kwa kulipa kodi zao.
“Hivi sasa nchi ipo katika mchakato wa kuandika Katiba Mpya, ninapenda kuwahakikishia Watanzania kuwa CCM itakuwa tayari kupokea maamuzi yoyote yatakayoamuliwa na wananchi.
“…. Na ikiwa mtaamua kuwa ya Serikali mbili, tatu hata tano sawa, lakini kubwa katika hili CCM hatuhitaji mchakato huu ufanyike kwa kuingiliwa kwa shinikizo kutoka kwa vyama vya upinzani au hata taasisi ambazo zimejificha kwa mlango wa nyuma.
“Sisi tulisema wazi tunapenda tuendelee na Serikali mbili, lakini katika hili tambueni kuwa na Serikali nyingi zaidi kuna hatari ya kuingia katika mifarakano na hata vita,” alisema Kinana.
Katibu Mkuu huyo alisema kuwa hatua ya baadhi ya watu kupita na kupandikiza chuki kuhusu Katiba Mpya, mawazo yao yanatakiwa kupimwa, kwani watu hao wana lengo la kuvunja badala ya kuimarisha umoja.
“Ni muhimu kuandika Katiba mpya ambayo itasaidia kuweka misingi bora na imara ya uongozi, lakini si kuwa na Katiba yenye utitiri wa kila aina ya Serikali, hili hapana, ila ikiwa mtaamua nyie wananchi wenyewe sisi hatuna pingamizi,” alisema.
Mapema Agosti mwaka huu, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete, aliwataka wanachama wa CCM kujiandaa kisaikolojia na muundo wa Serikali tatu, ikiwa Watanzania wataamua hivyo.
Rais Kikwete alinukuliwa na vyombo vya habari kupitia vikao vya NEC mjini Dodoma, ambapo alisema mwaka 1992, kundi kubwa la wananchi lilipinga kuingia katika mfumo wa vyama vingi, lakini lilisikilizwa na nchi ikaingia kwenye mfumo huu

habari na udakuspecially .com 

No comments:

Post a Comment

TUPE MAONI YAKO