Sunday 13 October 2013

Na Mhaiki Andrew, Songea

TIMU ya soka ya Majimaji Fc ya Songea juzi imeziduka  na kuichapa Polisi Moro bao 1-0 katika mchezo wa ligi ya Taifa ya Daraja la kwanza, mechi hiyo ilifanyika kwenye uwanja wa Majimaji mjini hapa.

   Mchezo huo ambao ulikuwa muhimu kwa Wanalizombe kuweza kurudisha matumaini na imani kwa wapenzi, mashabiki na wanachama wao kutokana na kuanza kwa ligi hiyo kwa kusuasua na kupelekea kupoteza mechi mbili na moja kutoka sare na Kimondo ya Mbeya.

    Majimaji ambayo ilianza mchezo huo kwa kasi kwa kulisakama kwa kulishambulia  lango la wapinzani wao ambao walionekana kucheza kwa kujiamini zaidi, tofauti na mchezo wao uliopita  na Mlale JKT ambapo maafande hao wa Polisi Moro  waliibuka na ushindi wa bao 1-0 ugenini.

    Katika mchezo huo Majimaji waliweza kuwatoa kimasomaso  wapenzi, mashabiki na wanachama  wao katika dakika ya 43 na Sayuni Mtunjilwa baada ya kutokea piga ni kupige langoni mwa maafande hao ambao wanamatumani makubwa ya kurudi tena kucheza ligi kuu ya Bara, baada ya msimu uliopita wa ligi hiyo waliweza  walishuka Daraja.

   Kuingia kwa bao hilo maafande hao wa Polisi Moro walionekana kupagawa na kuanza kucheza rafu ambazo ziliweza kuthibitiwa na mwamuzi wa mchezo huo, Rashid Ndanje wa kutoka Dar es Salaam pamoja na kuendelea kucheza kwa kujiamini wakiamini watasawazisha bao hilo na kupachika jingine la ushindi na kujizolea pointi zote tatu na kujiweka katika mazingira mazuri ya kurudi tena kucheza ligi kuu msimu ujao.

    Polisi Moro hasira zao hazikuweza kuishia uwanjani ambapo uongozi wa timu hiyo akiwemo, Fikiri Hussein waliweza kumshambulia kwa kumpiga na kumjeruhi usoni, mmoja wa viongozi wa kamati tendaji ya chama cha mpira katika Manispaa ya Songea(SUFA), Francis Kasembe”Farao” wakati zikiwa zimesalia dakika 2 kumalizika kwa mpambano huo.

    Ilidaiwa na baadhi ya watazamaji wa mchezo huo kuwa kiongozi huo, Kasembe alivamiwa na kuanza kushambulia wakati akipita kukusanya mipira kutoka kwa vijana ambao wanaookotea mpira kwa kuhofia isije kupotea punde mwamuzi wa mchezo huo atakapopuliza filimbi yake ya mwisho wa kumaliza mchezo huo na kubaki kuwashangaza watazamaji kwa hatua ambayo waliochukua maafande hao.

 

No comments:

Post a Comment

TUPE MAONI YAKO