Wednesday 3 April 2013

Mwanafunzi kidato cha pili 'abebeshwa' mzigo wa kulea familia

 Kaimu Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Komnyang’anyo, Nadhiru Kinyama akizungumza na mwandishi wa Thehabari.com
Mwanafunzi Mwenjuma Magalu (16), mstari wa pili kulia wa Shule ya Sekondari Komnyang’anyo

Na Thehabari.com, Handeni

MWANAFUNZI wa kidato cha pili Shule ya Sekondari Komnyang’anyo, Mwenjuma Magalu (16) amejikuta akibeba mzigo wa kulea familia baada ya familia hiyo kutelekezwa na babayake.

Mwanafunzi huyo anayeishi katika Kijini cha Msasa amejikuta katika hali hiyo ngumu baada ya mama yake mzazi, Hadija Magalu kufariki dunia ambaye ndiye aliyekuwa akiihudumia familia hiyo baada ya mzazi mwenzake (mumewe) kuitelekeza miaka minne iliyopita.

Mama huyo (Hadija Magalu) alifariki dunia Agosti, 2013 kwa matatizo ya uzazi na kuiacha familia hiyo ya watoto watatu aliyokuwa akiihudumia chini ya ulezi wa mamayake mzazi, Bibi Amina Mohamed.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi hivi karibuni kijijini Msasa, mwanafunzi Magalu alisema amelazimika kuilea familia hiyo baada ya bibi yake aliyeachiwa familia hiyo kuugua ugonjwa wa TB na kushindwa kuendesha shughuli za kilimo na nyinginezo kuisaidia familia hiyo.

“Bibi ndiye aliyekuwa akitupikia, tutafutia chakula na tulikuwa tukishirikiana naye hata kulima…lakini kazi hizo zote kutokana na afya yake hawezi kuzifanya, ninalazimika kuzifanya mwenyewe. Japokuwa nipo shuleni lakini natakiwa kujua tutakula nini tunapata wapi pesa ya chakula na shughuli nyingine za familia,” alisema Magalu akizungumza na mwandishi wa habari hizi.

Alisema familia yao hutegemea kilimo lakini wakati mwingine hulazimika kwenda kutafuta vibarua vya kufanya ili kupata pesa ya kula yeye pamoja na bibi yake. Aidha aliongeza kuwa wadogo zake wawili ambao awali alikuwa akikaa nao amelazimika kuwapeleka kwa mjomba wake baada ya kuona hali ni ngumu. Hata hivyo alisema wajomba zake nao hali yao ni ngumu hivyo wanashindwa kuhudumia familia hiyo.

Akizungumzia hali ya maisha ya familia hiyo Bibi. Amina Mohamed ambaye kwa sasa ni mgonjwa wa TB alikiri mwanafunzi huyo kuwa na majukumu mazito ya familia ambayo awali alikuwa ameyabeba yeye baada ya mwanaye kufariki dunia.

“Kweli mtoto huyu anaelemewa na malezi ya familia hii lakini sina cha kufanya kwa kuwa mimi ni mgonjwa wa TB na nimeshauriwa nisifanye kazi kwa sasa, hivyo kuanzia kupika, kulima shambani na hata kutafuta cha kula anafanya yeye baada ya kurudi shuleni,” alisema bibi huyo.

Mwanafunzi huyo ambaye anasomeshwa na msamaria mmoja aliyejitokeza baada ya familia yao kushindwa kumlipia ada amewaomba watu walioguswa na maisha ya familia hiyo kumsaidia.

Akizungumza hivi karibuni Kaimu Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Komnyang’anyo, Nadhiru Kinyama alikiri hali ngumu kwa kijana huyo kutokana na mazingira ya familia yao na kuongeza anahitaji kusaidiwa hata fedha za kujikimu na gharama zingine za masomo.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAONI YAKO