Tuesday 18 December 2012

Stendi ya Mkoa hali tete....

ABIRIA wamekwama katika Kituo cha Mabasi yaendayo mikoani kilichopo Ubungo jijini Dar es Salaam, baada ya nauli kuendelea kupanda.Imekuwa kawaida kwa wamiliki wa mabasi kupandisha nauli katika kipindi cha kuelekea katika sherehe za Sikukuu ya Chrismasi na Mwaka mpya .

Kutokana na kupanda kwa gharama hizo abiria wameirushia lawama Mamlaka ya Usafirishaji wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), kushindwa kusimamia tatizo hilo.

Ubungo kwa sasa kuna songamano wa abiria wakiwa wamekwama katika kituo hicho cha mabasi, ambapo nauli zilikuwa zimepanda hususan katika mabasi yaendayo Arusha, Tanga, Kilimanjaro.

Mabasi yaendayo Arusha na Kilimanjaro nauli zimefikia kiasi cha Sh30,000,kutokana na wingi wa watu wanaohitaji usafiri huo, huku magari ya Tanga nayo yakipandisha nauli mpaka Sh15,000, kutoka Sh12,000.

Mmoja wa abiria Joseph Kihiyo alisema wamekuwa wakiamua kurudi nyumbani kutokana na bei zinazotozwa katika mabasi hayo kwa kuwa haziendani na bei za awali hivyo zimewakwamisha safari yao.

“Kila wakala humu ndani ana bei yake, yaani kwenda hapo Korogwe ninaambiwa nitoe Sh15,000 wakati awali nilikuwa nikitumia Sh12,000 tu, “alisema Kihiyo.

Alieleza kuwa kipindi hiki cha sikukuu hizo kumekuwa na tabia ya ulanguzi wa tiketi kwa kuwa kila mtu anapewa tiketi kwa kiasi chake cha pesa alichotoa. Abiria mwingine Mussa Said alilalamikia hali ya kusumbuliwa katika masuala ya usafiri kwa kuwavuta vuta na hata muda wingine kuwaibia wakati wakiwalazimisha kupanda kwenye mabasi hayo.
 

“Humu ndani kuna tabia za ajabu sana unaweza ukawa unavutwa ukasema unapokelewa vizuri kumbe wengine wamekuja kuiba,” alisema Said.

Katibu Mkuu wa Chama cha Mawakala Ubungo (Cmmu), Hamisi Maneno alisema matukio yanayotokea kila siku katika kituo hicho yanasababishwa na kutokuwa na ushirikiano kati yao na wamiliki wa mabasi pamoja na Sumatra.

“Kama kungekuwa na ushirikiano wa Sumatra na wamiliki wa mabasi kwa kukaa na kutambua matatizo yanyotukabili, hili suala la ulanguzi wa tiketi lingekuwa limekwisha, lakini hakuna ushirikiano wowote na ndiyo maana mambo yanazidi kuwa mabaya,” alisema Maneno.

Maneno alisema ni jambo la aibu kwa nchi kama Tanzania iliyofikisha miaka 51 ya Uhuru lakini bado ina ubabaishaji katika sekta ya usafirishaji wa nchi kavu.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAONI YAKO