Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dk. Fenella Mukangara  (kulia) akimsikiliza Mwenyekiti wa kikundi cha Nyakalalo kililopo  kijiji cha Kitigiri wilayani Geita, Gideon Msabila (kushoto)  ambaye alimuelezea jinsi walivyonufaidika na mkopo wa mfuko wa maendeleo ya vijana fedha ambazo zimewawezesha kufungua duka  la rejareja la bidhaa za nyumbani. 
Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dk. Fenella Mukangara  (kulia) akiangalia  nguo zinazoshonwa na kikundi cha ushonaji kilichopo kijiji cha  Bugalama  wilayani Geita ambacho kimenufaika na mkopo wa  shilingi milioni mbili kutoka mfuko wa maendeleo wa halmashauri hiyo. Waziri Dk. Mukangara  alitembelea kijiji hicho jana ili kuona fedha za mkopo zimewasaidiaje vijana kujikwamua kimaisha. 
Vijana wa kikundi cha kusaidiana kulima cha Busaka katika kijiji cha Kitigiri wakifurahia fedha shilingi 50,000/= walizopewa na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dk. Fenella Mukangara  (wanne kulia) kwa ajili ya kununulia soda za sikukuu ya Krismasi . Waziri Dk. Mukangara  aliwahimiza vijana hao kujiunga kwenye vikundi vya maendeleo vya kilimo ili weweze kupata mkopo wa kununulia pembejeo na kuweza  kuzalisha chakula kwa wingi zaidi.
Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dk. Fenella Mukangara  (wanne kulia) akiongea na vijana wa kikundi cha kusaidiana kulima cha Busaka kilichopo kijiji cha Kitigiri  wilayani Geita umuhimu wa kujiunga kwenye vikundi vya maendeleo vya kilimo ili weweze kupata mkopo wa kununulia pembejeo na kuweza  kuzalisha chakula kwa wingi zaidi . 
Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dk. Fenella Mukangara  (kulia) akimsikiliza Mwenyekiti wa kikundi cha Bodaboda kilichopo kijiji cha  Bugalama  wilayani Geita,  Enos Komanya  wakati alipotembelea kikundi hicho ambacho kilipata mkopo  kutoka mfuko wa maendeleo wa halmashauri. Waziri Dk. Mukangara  alitembelea kijiji hicho jana ili kuona fedha za mkopo zilizotolewa na mfuko wa maendeleo ya vijana zimewasaidiaje vijana kujikwamua kimaisha.
Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dk. Fenella Mukangara  (wanne kulia) akiwa katika picha ya pamoja  na viongozi wa wilaya ya Geita, Kata ya Bukondo na  kijiji cha Kitigiri mara baada ya kumaliza ziara yake katika kijiji  hicho ili kuona fedha za mkopo za mfuko wa maendeleo ya vijana  zimewasaidiaje vijana kujikwamua kiuchumi.(Picha na Anna Nkinda – Maelezo).

Na Anna Nkinda – Maelezo, Geita
Vijana  wametakiwa kushiriki katika suala la ulinzi na usalama wa maeneo wanayoishi kwa kujiunga na vikundi vya ulinzi shirikishi ili kulinda na kusimamia rasilimali za vijiji vyao.
Hilo litafanikiwa endapo vijana  watakuwa na moyo wa kujituma  na kutambua kuwa wanajukumu la kujenga taifa kwa kuhakikisha kuwa wanajiletea maendeleo yao na nchi kwa ujumla kutokana na  kazi mbalimbali wanazozifanya.

Rai hiyo imetolewa  mjini hapa jana  na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dk. Fenella Mukangara  wakati akiongea kwa nyakati tofauti na wanavikijiji vya Bugalama na Kitigiri vilivyopo wilayani Geita alipozitembelea baadhi ya Vyama vya Kuweka Akiba na Kukopa (SACCOS) zilizopata mkopo  kupitia mfuko wa maendeleo wa vijana na fedha za maendeleo ya mfuko wa Halmashauri.

Dk. Mukangara alisema kuwa maendeleo ya nchi yanawategemea vijana ambao ndiyo nguzo ya taifa  hivyo basi wizara yake kupitia halmashauri za wilaya itahakikisha kuwa inatoa mafunzo ya kuwajengea uwezo vijana jambo la muhimu ni kujiunga katika vikundi vya maendeleo ili waweze kufikiwa kwa urahisi.  
“Uongozi wa kijiji uhakikishe kuwa  unawahimiza  vijana na kuwajengea  uwezo katika mtazamo wa kujitengemea, kujituma na kufanya kazi na  kujiunga kwenye vikundi vya maendeleo  ili iwe rahisi kupata mkopo kupitia SACCOS zilizopo vijijini mwenu” alisema Dk. Mukangara.

Aliwataka wanakijiji hao  kuwasimamia vijana wao ili wanawajibike na  kutambua  kuwa wanajukumu kubwa la kuhakikisha kuwa wanashiriki katika shughuli za kilimo cha chakula na biashara jambo ambalo litasababisha kuwa na chakula cha kutosha na kuepukana na janga la njaa.

Dk. Mkangara alisema,  “Najua nyinyi ni wakulima wazuri ila mnatakiwa kuboresha kilimo chenu ili muweze kuzalisha mazao mengi na ya ziada , vijana wenu  washiriki katika kilimo hasa cha mazao ya biashara na siyo kuwaachia wazee peke yao, wawe tayari kujituma na kuhakikisha kuwa chakula wanachokula wamekitolea jasho kwa namna moja au nyingine”.

Naye Mwenyekiti wa Kikundi cha Bucha la nyama ya ng’ombe ambacho kilipata mkopo wa shilingi milioni mbili kutoka SACCOS ya Bugalama  Mathias Lucas alisema kuwa mkopo walioupata umewawezesha kupanuka kwa biashara na mtaji, kuongezeka kwa wanachama kutoka wanne hadi kumi  na kujenga bucha kubwa la kuuzia nyama.
“Mkopo tulioupata umetusaidia kujikwamu kiuchumi na kuweza kukabiliana na hali ngumu ya maisha , tumeweza  kuwaajiri na vijana wengine ambao hawakuwa na ajira lakini tunakabiliwa na changamoto ya kutokuwa na mtaji wa kutosha na kufungwa kwa mnada wa ng’ombe wilayani Geita .

Tunaiomba Serikali iweze kutuongezea fedha ya mtaji kwa kutupatia mkopo mkubwa zaidi  na  tupewe mafunzo ya ujasiriamali ili tuweze e kujua umuhimu wa kuweka akiba na kukopa”, alisema Lucas .
Akisoma taarifa ya  kikundi cha Tupendane  ambacho  kilipata mkopo wa shilingi 1,400,000/= kutoka SACCOS ya Vijana Bukondo na kujishughulisha na  kazi za ushonaji wa  nguo za kike mwenyekiti wa kikundi hicho Meshaka Philipo alisema kuwa wamefanikiwa kuajiri mafundi cherehani vijana watatu na kuuza nguo kwa wanakijiji na hivyo kupata fedha za kuinua mtaji wao.

Philipo alizitaja changamoto zinazowakabili kuwa ni pamoja na mtaji mdogo, elimu duni ya utunzaji wa kumbukumbu za fedha na ujasiliamali, upungufu wa vitendea kazi kwa ajili ya ushonaji na usafiri ambao ni baiskeli kwa ajili ya kupeleka nguo kwenye masoko ya nje ya kijiji.
Katika kijiji cha Bugalama waziri Dk. Mukangara alitembelea vikundi vya Bucha, Bodaboda na ushonaji ambavyo vilipata mkopo kutoka SACCOS ya kijiji hicho kutipia mkopo wa halmashauri ya wilaya ya Geita wa shilingi milioni tano na katika kijiji cha Kitigiri alikagua vikundi vya Tupendane na Nyakalalo ambavyo vilipata mkopo kutoka SACCOS ya Vijana Bukondo ambayo ilipata shilingi milioni tano kupitia mfuko wa maendeleo ya vijana.