Saturday 5 January 2013

Shamrashamra za miaka 49 ya Mapinduzi zaanza rasmi!

SHEREHE za kutimiza miaka 49 ya Mapinduzi ya Zanzibar, zinaanza rasmi leo kwa viongozi wa kitaifa kufanya kazi ya usafi wa mazingira katika wilaya zote za Unguja na Pemba. Kwa mujibu wa ratiba, iliyotolewa na kamati ya sherehe na maadhimisho ya kitaifa, imeonyesha miradi ipatayo 62, inatarajiwa kuzinduliwa.

Ratiba hiyo, imeonyesha Rais Jakaya Kikwete, atafungua Shule ya Sekondari ya Mlimani, iliyopo Matemwe Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein(pichani), atazindua miradi mbalimbali, ikiwemo ufunguzi wa jengo la Chuo cha Utawala wa Umma katika Tunguu Wilaya ya Kati Unguja.

Pia atafungua mradi wa E-Government katika Wilaya ya Magharibi Unguja na kufungua Skuli mpya ya Sekondari ya Umoja, iliyopo Uzini.

Pia atafungua mradi wa kuhama kutoka Teknolojia ya Analojia kwenda Dijitali na ufunguzi wa studio ya kurikodia Sanaa na Muziki, ambapo kwa upande wa Pemba atafungua Sekondari ya Sekondari ya Shamiani.

Mbali na shughuli hizo, siku ya kilele hapo Januari 12 kwenye Uwanja wa Amani, Rais Shein atakagua gwaride lililoandaliwa na vikosi vya ulinzi na usalama.

Naye, Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Shariff Hamad, atafanya uzinduzi shule na maabara, wakati Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Idd atafanya shughuli kama hizo kwa ufunguzi wa shule na majengo mapya ya nyumba za wazee zilizopo Sebleni.

Katika shamrashamra za kutimiza miaka 49, baadhi ya marais wastaafu, mawaziri mbali mbali wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Muungano, watafanya shughuli za ufunguzi wa miradi mingine.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAONI YAKO