Monday 10 June 2013

K'NJARO UPDATE: TAVETA ATHLETICS CHAMPIONSHIP YAIINUA TANZANIA

TUKIO HILI LIMEFANYIKA JUMAMOSI YA JUNI 8, 2013 KATIKA WILAYA YA TAVETA, KAUNTI YA TAITA-TAVETA, KATIKA MKOA WA PWANI.

 BARAKA WILLIAM MTANZANIA KUTOKA KLABU YA HOLILI ATHLETICS (HYAC) AKIMALIZA MBIO ZA MITA 5000 NA KUIBUKA SHUJAA KWENYE MBIO NYINGINE ZA MITA 1500.

Katika kuhakikisha riadha nchini Tanzania inafuta uteja kwa wakimbiaji wake kwa wafukuza upepo wa Kenya, Klabu ya Holili (HYAC) ya Mkoani Kilimanjaro imedhihirisha hilo katika Taveta Athletics Championship kwa kuwabwaga Wakenya katika mbio za meta 5000, 1500, 800 na 100.

Michuano hiyo ya Taveta imefanyika mwishoni mwa wiki katika Kaunti ya Taita-Taveta katika Mkoa wa Pwani nchini Kenya katika wilaya ya Taveta kwa kuwakutanisha wanariadha wa nchini Kenya huku Holili Youth Athletics Club ikialikwa kutoka nchini Tanzania.

Katika Mbio za meta 5,000 alikuwa ni Baraka Williams aliyekimbia kwa dakika 14:45:22 nafasi ya pili ikishikwa na Mtanzania mwingine Abubakar  Joel aliyekimbia kwa muda wa 16:00:00  na nafasi ya tatu ikashikwa na Mkenya Kivoko Makao ambaye alikimbia kwa muda wa 16:34:00.

Wambura Lameck, Mtanzania kutoka katika klabu ya Riadha kwa vijana (HYAC) alionyesha uwezo katika mbio za meta 100 na 800 kwa wanaume; katika mbio za meta 100 Wambura alikimbia kwa muda wa sekunde 12:67 akiwatupa Wakenya Walter Kamujalo (13:12), Emmanuel Paulo (13:70) na Joseph Daudi (14:20).

Mbio za mita 800 Wambura Lameck alikimbikia kwa muda wa dakika 2:02:16 akimwacha Mkenya Ropya Nyingi ambaye alichukua muda wa dakika 2:04::14 na nafasi ya Tatu ikishikwa na Mtanzania kutoka HYAC Paulo Jackson aliyekimbia kwa muda wa dakika 2:05:98, Wakenya wengine Joseph Daudi (3:00:00) na Philip Matheka (3:04) walishika nafasi mbili za mwisho.

Pia Watanzania waliwaonyesha kazi nyingine Wakenya katika mbio za meta 1500 pale Baraka Williams kutoka HYAC alipowakimbiza na kuongoza baada ya kumaliza kwa muda wa dakika 3:48:77 akifuatiwa na Mkenya Vicent Daniel kutoka Taveta aliyemaliza kwa kutumia muda wa dakika 4:16:85 nafasi ya tatu ikishikwa na Mtanzania mwingine kutoka HYAC Paulo Jackson ambaye alikimbia kwa dakika 5:04:66 na Mkenya Tumuna Ludovick akikimbia kwa muda wa dakika 5:09:07.

Kwa upande wa wanawake Watanzania Furaha Sambeke na Pendo Pamba walifanya kweli katika meta 800 kwa kushika nafasi mbili za juu. 

Furaha Sambeke anayenolewa na Klabu ya Holili Youth Athletics alikimbia kwa muda wa dakika 2:30:00 na Pendo Pamba akimaliza kwa dakika 3:10, nafasi ya tatu ilishikwa na Mkenya Emily Wamboi na ya nne ikishikwa na Mkenya mwingine Cecily Kimale ambao wote walikimbia kwa muda wa dakika 3:22:00 na 4:12:00.

Akizungumzia ushindi huo Katibu wa klabu ya Holili Youth atletics, Innocent Mlashane, wapongeza wanariadha hao kwa ushindi mkubwa  waliouonesha kutoka kwa wapinzani wao na kuahidi kuwa kamwe hawatarudi nyuma.

“Changamoto tuliyonayo kubwa ni kupata wafadhili hasa wa kuweza kuwahudumia wachezaji wetu ambao kwa sasa wako katika kambi ya Tarakea, na mchezo waliocheza hapa taveta inaonesha kuwa tuna wachezaji wazuri hivyo tukipata msaada zai naamini tutasonga mbele zaidi” alisema

Alisema klabu ya holili imedhamiria kurudisha heshima ya Tanzania kwa nguvu zote hasa katika mchezo wa riadha ambao kwa serikali wameonesha kuusahau.

Taveta Athletics Championship imefanyika ikiwa na makusudi ya kutengeneza Timu ya Riadha ya Taifa la Kenya ambako mchujo rasmi utafanyika Mjini Mombasa kwa watanzania walioshinda katika mbio hizo nao watakuwemo katika kinyang’anyiro hicho kwa ajili ya kupata uzoefu zaidi kutokana na ukweli kwamba taifa la Kenya limekuwa bora katika riadha barani Afrika.

Mwandishi: JOHNSON JABIR, Moshi-Kilimanjaro

No comments:

Post a Comment

TUPE MAONI YAKO