Thursday 2 May 2013

Kibarua wa shirika la umeme Ruvuma afariki baada ya kunaswa na umeme

Picha sio ya tukio halisi
 ............................................................
Na nathan Mtega,Songea.

KIBARUA mmoja wa Shirika la umeme Tanzania (Tanesco) Mkoa wa Ruvuma  Sandari Sandari (35) amekufa papo hapo baada ya kunaswa na umeme akiwa juu ya nguzo ya umeme wakati alipokuwa akibadilisha nyaya katika eneo la madizini katika Manispaa ya Songea.

Habari zilizopatikana  na zimethibitishwa na kamanda wa polisi wa Mkoa wa Ruvuma  Deusidedit Nsimeki zimeeleza kuwa tukio hilo limetokea jana majira ya saa kumi jioni katika eneo hilo la madizini kata ya Lizaboni ambako  Sandari akiwa juu ya nguzo ya umeme alikumbwa na kifo hicho baada ya umeme kuwashwa ghafla.

Alifafanuwa kuwa inadaiwa siku ya tukio Sandari ambaye ni kibarua wa Tanesco alikwenda kwenye eneo la Madizini ambako kulikuwa na hitilafu ya umeme na alipofika na kuanza kazi alilazimika kupanda juu ya nguzo kwenda kubadilisha nyaya.

Alieleza kuwa akiwa juu ya nguzo akibadilisha nyaya hizo za umeme ghafla alinaswa na umeme na kumsababishia kifo papo hapo ambapo chanzo cha tukio hilo kimetokana na hitilafu ya mfumo wa umeme.

 Meneja wa Tanesco Mkoa wa Ruvuma  Mhandisi Stephen Manda akizungumza na Radio One Stereo kwa njia ya simu alithibitisha kutokea kwa tukio hilo ambalo alidai kuwa limetokana na hitilafu ya mfumo wa umeme kwenye eneo hilo.


Chanzo: www.demashonews.blogspot.com

No comments:

Post a Comment

TUPE MAONI YAKO