Tuesday 14 May 2013

WAZEE WAZINDUA SHIRIKA LAO LA MT. AGUSTINO


Rais wa baraza la maaskofu Tanzania akiwa na wazee wa shirika la Mt. Agustino nje ya Kanisa la moyo Mt. Yesu Parokia ya Kihesa jimbo la Iringa mara baada ya Misa ya uzinduzi hii leo

Baadhi ya wazee wa shirika la Mt. Agustino wakiwa nje ya Kanisa.

Mhashamu askofu Tarcisius Ngalalekumtwa akiongea na wazee nje ya Kanisa.

==============================================
Na Gustav Chahe

RAIS wa Baraza la Maaskofu Tanzania Mhashamu Tarcisius Ngalalekumtwa amesema wazee wasisahaulike katika huduma muhimu ili waendelee kutoa mang’amuzi yao mbalimbali katika jamii.

Mhashamu askofu ameyasema hayo katika maadhimisho ya Misa Takatifu iliyokuwa maalum kwa uzinduzi wa shirika la wazee na wastaafu mbalimbali la Mtakatifu Agustino iliyofanyika katika Kanisa la Kiaskofu la Moyo Mtakatifu wa Yesu Parokia ya Kihesa jimbo la Iringa hii leo.

Amesema wazee ni tunu ya familia na hivyo kuwatenga wazee hao ni kumkosea Mungu kwa kuwa wao ndio mashahidi wa misingi ya Baraka.

Askofu Ngalalekumtwa ambaye pia ni askofu wa jimbo la Iringa amesema ndio wanaoendeleza mapokeo mbalimbali yaliyo katika misingi ya maadili na kuongeza kuongeza mang’amuzi ya changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii ya watanzania.

Amesema wazee wahudumiwe kwa upendo bila kubaguliwa na wapewe haki stahiki bila kusumbuliwa kwa kuwa ni haki yao kupata mahitaji muhimu kama walivyo wengine.

“Kanisa linashuhudia uwepo wa Yesu Kristo na hawa wazee ndio mashahidi wa misingi ya wokovu na Baraka za Mungu. Wahudumiwe bila kubaguliwa” amesema.

Vile vile amesema katika familia wazee wanarithisha tunu za familia hasa katika maadili na mafundisho yenye hekima na busara.

Hata hivyo ameitaka jamii kuwa na upendo kwa rika mbalimbali ambazo zipo katika jamii kwa kuwa upendo ndicho kiini cha imani na amani.

“Upendo unalea, unaleta nguvu, unafariji na ndicho chanzo cha amani na furaha kwa binadamu anayehitaji kufarijiwa na kuhudumiwa sawasawa na mwingine” amesema.

Amesema tunu za nchi ambazo ni zawadi ya kutoka kwa Mungu ziwanufaishe wazee ambao kwa namna moja au nyingine ndio washauri wa mambo mbalimbali na pale wanapohitaji haki zao kusiwe na ubabaishaji.

Ubabaishaji wa makusudi katika utoaji huduma ni kinyume na haki za binadamu ambao ni haki yao kupata huduma.

Amewataka viongozi mbalimbali walio na mafundisho ya kikristo kutumia mafundisho ya upendo katika kuihudumia jamii bila kujali rika na hasa kuwapa kipaumbele wazee ambao umri wao umekwenda.

Naye Mwenyekiti wa shirika hilo William Myonga amesema lengo la kuanzisha shirika hilo ni kuwaunganisha wazee kwa ajili ya kutathimini yale yaliyowakumba wakati wa ujana.

Amesema yapo mengi ambayo katika ujana yamekuwa kikwazo kwao kiasi cha kusababisha kumtumikia Mungu ipasavyo na hivyo kupitia shirika lao watapata nafasi ya kukumbushana na kumuomba Mungu.

Mhamasishaji wa shirika hilo Licas Mwasimile amesema wanakabiliwa na changamoto mbalimbali hasa katika kupokelewa katika majimbo mbalimbali.

Mwasime amesema changamoto mojawapo ni pale wanapohamasisha na kuambiwa kuwa shirika halitambuliwi kitaifa licha ya kuwa elimu na maelezo juu ya kulitangaza shirika hilo yanajitosheleza.

Ametoa kilio cha wazee hao kwa baraza la baaskofu kuwasaidia kupokelewa kwa urahisi katika majimbo yao ili kuwawzesha utume wao kuwa mwepesi.

Shirika la Mtakatifu Agustino limeshafika katika majimbo 22 ambapo kwa kanda ya nyanda za juu kusini limeshaingia katika majimbi ya Mbeya, Mbinga, Songea na Iringa.

Mlezi wa shirika hilo Padre Gregory Mashtaka amewataka wazee wa shirika hilo kuwa na mshikamano pamoja na mawasiliano.

“Si kwamba mmekwisha kufika, huu ni mwanzo tu. Hali yetu ni ya uzee. Hivyo, tuipokee kwa furaha” amesema Pd. Mashtaka.

Amewataka wazee hao kuwa washiriki walio hai na si hoi kwa kuishi kwa ushirikiano na kuwa na maisha ya utakaso.

Katika uzinduzi huo, jumla ya wazee 89 walipokelewa katika shirika hilo la Mtakatifu Agustino.source mzee wa matukio Iringa.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAONI YAKO